Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuapishwa rasmi hapo tarehe 9 Aprili 2013
Wananchi wa Kenya wanasema, mchakato wa uchaguzi umekwisha na Rais Uhuru Kenyatta
ameshinda kihalali, sasa wananchi wa Kenya wanapaswa kuunganisha nguvu zao kwa ajili
ya kujenga uchumi wa nchi. Rais Uhuru Kenyatta aliyeshinda uchaguzi mkuu dhidi ya
mpinzani wake mkuu Raila Odinga anatarajiwa kuapishwa kuwa Rais wa Kenya hapo tarehe
9 Aprili 2013, kadiri ya taarifa zilizotolewa na Shirika la habari la Reuters.
Jeshi
la Polisi nchini Kenya limekwishawatia pingu watuhumiwa 23 waliokuwa wanajihusisha
na uchochezi na vurugu hivi karibuni mara baada ya Mahakama kuu ya Kenya kutangaza
kwamba, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ameshinda kwa kupata kura halali. Wananchi wa
Kenya wanaendelea kuhimizwa kulinda na kudumisha haki na amani na kwamba, vurugu,
chuki na uhasama havina nafasi tena, kwa watu wanaoitaka kucharuka kwa maendeleo kwa
sasa.
Pamoja na hali ya amani na utulivu kurejea tena katika maeneo mbali
mbali nchini Kenya, lakini, Mombasa bado hali si shwari sana kutokana na baadhi ya
wananchi kuendeleza azma ya kutaka kujitenga kutoka Kenya. Hii ni kutokana na matatizo
ya ardhi na hali mbaya ya kiuchumi wanayokabiliana nayo wananchi wa eneo hili.