2013-04-02 11:06:29

Imegota miaka 8 tangu alipofariki dunia Papa Yohane Paulo II


Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya miaka minane, tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipofariki dunia kunako tarehe 2 Aprili 2005, baada ya kufanya hija ya maisha ya kiroho, akiubeba Msalaba wake na kuendelea kumfuasa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Kardinali Jorge Mario Bergoglio, ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko, aliteuliwa na Papa Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu kunako mwaka 1992 na mwaka 2001 akamteuwa kuwa Kardinali.

Kardinali Bergoglio akihubiri katika Ibada ya Misa Takatifu, Mei Mosi 2011, kwenye Kanisa kuu la Buenos aires, Argentina, wakati Mama Kanisa alipokuwa anamtangaza Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa Pili kuwa Mwenyeheri, alisema kwamba, Kanisa lilikuwa linashangilia na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa zawadi kubwa ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili.

Ni kiongozi aliyeonesha ujasiri wa pekee katika kupambana na mifumo kandamizi, akawaimarisha ndugu zake katika imani kwa njia ya hija zake za kichungaji, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake; ushuhuda amini wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alitumaini kwa namna ya pekee huruma ya Mungu katika maisha na utume wake. Alithubutu kuwaalika waamini kuondokana na woga na badala yake wamfungulie Kristo malango ya mioyo yao!

Kardinali Bergoglio wakati akiadhimisha kumbu kumbu ya miaka miwili tangu alipokuwa amefariki dunia Papa Yohane Paulo wa pili alisema, kwa hakika, alikuwa ni kielelezo cha umoja wa Watu wa Mungu; Mtu wa sala, aliyetumia muda wake mwingi kwa ajili ya kusali na kuabudu Ekaristi Takatifu, mambo yaliyomkirimia nguvu ya maisha ya kiroho kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Ni kiongozi aliyejitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Mwenyeheri Yohane Paulo katika maisha na utume wake amekuwa kweli ni shahidi amini wa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.