2013-04-01 11:04:43

Watu waliofariki dunia kwa kuporomokewa Jengo Dar es Salaam wanazidi kuongezeka


Taarifa ya Serikali ya Tanzania iliyonukuliwa na Shirika la Habari la AP inabainisha kwamba, hadi kufikia Jumatatu asubuhi, tarehe Mosi, Aprili 2013, maiti 32 zilikuwa zimekwishatolewa kwenye Jengo lililoporomoka wiki iliyopita. Matumaini ya kuwapata watu waliofukiwa na kifusi wakiwa hai yanazidi kufifia. Inasikitisha kuona kwamba, Jengo hili lenye ghorofa 16 lililokuwa linakaribia kumalizika limekuwa ni chanzo cha vifo vya watu wasiokuwa na hatia, wakiwamo watoto waliokuwa wanacheza katika eneo hili.

Mashahidi wanasema, bado kuna watu wengi ambao wamefukiwa na kifusi katika jengo hili. Katika miaka ya hivi karibuni kuporomoka kwa majengo katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki linaonekana kuwa ni jambo la kawaida kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya wamiliki na makandarasi wanapindisha sheria na kutaka kubana matumizi, matokeo yake ni maafa kwa watu wasiokuwa na hatia!







All the contents on this site are copyrighted ©.