2013-04-01 10:09:39

Kristo Mfufuka awaongoze watu wote katika njia ya haki, amani na upendo


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe na baraka zake kwa mji wa Roma na Dunia katika ujumla wake, "Urbi et Orbi" mara baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili ya Pasaka, tarehe 31 Machi 2013 ameushukuru kwa namna ya pekee, umati wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, uliokuwa umefurika kwa wingi katika Ibada hiyo, bila kuwasahau wale ambao walikuwa wameunganishwa na Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa njia ya mawasiliano ya Kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwatakia watu wote Pasaka Njema. Anawaalika waamini na wote waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na viunga vyake kuwashirikisha wanafamilia wao ujumbe wa furaha, matumaini na amani; fadhila ambazo kila mwaka zinarudiwa na kuhimizwa na Mama Kanisa katika hija ya maisha na utume wake.

Kristo mfufuka ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti awe pia ni nguzo na faraja kwa wote wanaoteseka, wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini kwa ushuhuda wa uwepo na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Amewashukuru wananchi wa Uholanzi waliotoa zawadi ya maua yaliyotumika kupamba Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu, Siku kuu ya Pasaka.

Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kuwashangaza watu wengi kutokana na umati mkubwa wa watu wanaofika hapa mjini Vatican tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, anasema, Kristo Mfufuka awaongoze watu wote katika njia ya haki, amani na upendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.