Katika mwaka huu wa imani, Kanisa linaitazama familia kwa namna ya pekee kama kitalu
cha pekee kwaajili ya uinjilishaji wa kina katika jamii zetu. Ni katika familia tunapata
viongozi mbalimbali wa Kanisa na Taifa kwa ujumla. Kama familia zetu hazijakuwa katika
misingi bora ya kimaadili ni wazi kuwa huo ni mwanzo na chanzo cha mmomonyoko wa maadili
katika jamii. Wahenga wetu walikuwa
na misemo na methali nyingi ambazo ukizitafakari kwa kina zina mafunzo mengi katika
jamii yetu ya leo. Methali ambayo imenijia mara akilini mwangu ni hile isemayo “Mtoto
umleavyo ndivyo akuavyo”. Kama familia zetu hazina maadili mema, tutegemee pia kupata
viongozi wetu katika Nyanja zote wasiokuwa na maadili mazuri. Maadili mema ni
fadhila inayokua na kutengeneza mizizi katika maisha yetu sisi binadamu pale yanapofanyiwa
kazi. Hivyo ni dhairi kuwa kama familia zetu hazijajengeka katika misingi bora ya
upendo na utu mwema, hatuwezi kuwa na taifa lenye watu wenye kupendana, kujaliana
na kuthaminiana. Katika mwaka huu wa imani sisi wanafamilia tunaalikwa na Mama
Kanisa kutafakari kwa namna ya pekee mafundisho ya Kanisa kuhusu maisha ya familia
na changamoto mbalimbali tunazo kabiliana nazo. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya chombo
hichi cha Kanisa ambacho mara kwa mara kimekuwa na lengo la kutuongoza kwenye kweli
za maisha kwa lengo la kutaka kutuongoza vema kuelekea kwa muumba wetu. Tukitumia
zawadi hii vyema kamwe hatuwezi kupotea kwani Kristu mwenyewe ameahidi kuwa na Kanisa
lake “siku zote, hata ukamilifu wa dahari (Mt. 28:20) Katika Mtaguso wa Pili wa
Vatikani katika Konstitusio ya kichungaji juu ya Kanisa katika ulimwengu wa leo Mababa
wa Mtaguso walitafakari maisha ya ndoa na familia kwa kina na kutoa sura moja nzima
kwaajili ya kujadili maisha ya ndoa na familia na changamoto mbali mbali tunazo kabiliana
nazo katika ulimwengu wetu wa leo. Sauti na busara za Mababa wa Mtaguso huu zinaendelea
kuzungumza nasi katika maisha yetu ya kila siku. Baadhi ya changamoto zilizotolewa
katika mtaguso huo ni kuhusu tatizo la talaka, mitala, maisha ya mume na mke nje ya
ndoa na changamoto nyingine nyingi tunazokabiliana nazo. Mtaguso huo ulikuwa unafahamu
wazi umuhimu wa ndoa na maisha ya familia katika maisha ya Kanisa na ulimwengu kwa
ujumla. Hivyo basi, wakati wa mkutano wa Mtaguso ulikuwa wakati wa pekee wa kuweza
kuyamulika matatizo hayo kwa mwanga wa Injili. Jambo hilo lilifanyika kwa kuelezea
kwa kina maana ya ndoa na familia kutokana na uelewa wa Kanisa ambao msingi wake ni
ufununuo wa Kimungu kutoka katika Maandiko Matakatifu. Hatuwezi kuzungumzia maisha
ya familia bila kugusa maisha ya ndoa kwasababu ndoa ndio inayotengeneza maisha ya
familia. Katika siku hii ya leo ningependa tutafakari kwa pamoja kuhusu ndoa kama
ushirika wa maisha yote kati ya mume na mke na kadiri tutakapokuwa tunaendea kuitafakari
mada yetu tutaweza pia kutafakari jinsi ushirika huu ulivyoanza. Mwalimu wangu
wangu alinifundisha kuwa ninaposoma kwaajili ya kujiandaa na mitihani niandae ufupisho
au muhtasari wa kile ninachokisoma kusudi niweze kukumbuka kiuraisi. Tunaweza kutoa
maelezo mengi kuhusu manna ya ndoa lakini katika maelezo yote tunaweza kupata sentensi
fupi ya ufupisho inayoweza kutupa maana ya ndoa. Tunaweza kuielezea ndoa kwa ufupi
kama ushirika wa maisha yote kati ya mume na mke. Tukisoma sharia za Kanisa kifungu
cha 1055 tunaweza kupata maelezo mazuri sana kuhusu maana ya ndoa. Kifungu hiko kinaelezea
ndoa kama agano kati ya mume na mke wenye lengo la kutengeneza ushirika wa kudumu
na ushirika huu unajengwa katika msingi wa upendo kati ya wenzi wawili, kushiriki
katika kazi ya uumbaji na kuhakikisha kuwa zawadi ya watoto watakaojaliwa wanapata
elimu bora itakaowasaidia kukua katika misingi bora ya kimaadili. Katika uelewa
wa ndoa katika Kanisa kuna vipengele viwili ambavyo siku zote inabidi kuvikumbuka,
navyo ni hivi: ndoa inayotambulika kikanisa, inatengeneza umoja usioweza kutenganishwa
na binadamu yeyote. Katika tafakari yetu ya leo na tunavyoendelea kuutafari mwaka
huu wa imani. Tuziombee familia zote zilizo katika utengano na magomvi ya hapa na
pale kusudi upendo wa Mungu ukapate kuzishukia, zikapate kuunganika tena na zile zilizokuwa
na ugomvi zikapate kuwa na maelewano. Makala hii imeandaliwa na Shemasi Titus
Nkane OSB.