2013-04-01 10:43:52

Adhimisho la Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya furaha, amani upendo na mshikamano wa dhati!


Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu, katika mahubiri yake kwenye Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, yaliyofanyika kwenye Kaburi Takatifu la Yesu mjini Yerusalemu, hapo tarehe 31 Machi 2013, amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Pasaka yenye kheri na baraka tele katika maisha yao! Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya furaha ya kweli, amani, upendo na matumaini mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka.

Kaburi wazi ni kielelezo cha imani kwa Kristo mfufuka, imani ambayo waamini wanapaswa kuirutubisha kwa kujenga na kuimarisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na ushuhuda wa matendo ya huruma, hasa kwa wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ufufuko wa Kristo ni kiini cha Imani ya Wakristo, changamoto ya kuendeleza umoja na majadiliano ya kiekumene, ili siku moja waweze kuwa chini ya Mchungaji na Imani moja.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kiwe ni kipindi cha kukabiliana na changamoto mbali mbali za kiimani kwa ujasiri na matumaini mapya. Changamoto zilizoko mbele ya waamini kwa wakati huu ni pamoja na: Uinjilishaji mpya unaopaswa kujipambanua kwa njia ya huduma kwa maskini na ushuhuda wa nguvu ile ya upendo wa Kristo inayotenda kazi ndani mwao kama anavyofanya kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko. Kuchaguliwa kwake ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa watu wa nyakati hizi.

Mchakato wa Uinjilishaji Mpya anasema Patriaki Twal unajikita hasa katika hija ya pamoja inayofanywa na waamini, huku wakidumisha udugu, umoja, upendo na mshikamano wa dhati; daima wakijitahidi kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka. Kanisa la Mwanzo lilijengeka na kuimarika kwa njia ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma, changamoto ya kuendeleza mshikamano wa kidugu, hata kiasi cha kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kanisa Mashariki ya Kati linateseka na kukabiliwa na changamoto na fursa mbali mbali zinazoweza kupata majibu ya kina kwa njia ya ushuhuda wa imani. Waamini waendelee kuonesha mshikamano na wakimbizi, wahamiaji na wote wasiokuwa na makazi maalum kutoka Syria na nchi ambazo bado kinzani na migogoro ya kijamii inaendelea kufuka moshi. Pasaka ya Kristo Mfufuka iwe ni chemchemi ya furaha kwa Wakristo wote hata katika shida na mahangaiko yao ya kila siku. Hata baada ya Ufufuko wa Kristo, bado waamini wataendelea kubeba na kuandamana na Misalaba ya Maisha yao kwa imani, matumaini na mapendo.

Waamini wanachangamotishwa kwa namna ya pekee, kama alivyosema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kuinua macho yao juu ya Msalaba wa Kristo, ili wapate kumwona na kumshuhudia Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anaonesha ubinadamu na umungu wake, chemchemi ya matumaini ya Kikristo!

Patriaki Twal anasema katika mahubiri yake kwamba, ana uhakika mkubwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, licha ya kusali na kutafakari kwa ajili ya Kanisa, ataendelea pia kuombea: misingi ya haki, amani na upatanisho katika Nchi takatifu. Amehitimisha mahubiri yake ya Siku kuu ya Pasaka kwa kuwatakia watu wote amani na Pasaka Njema.







All the contents on this site are copyrighted ©.