2013-03-31 09:26:01

Ushuhuda wa wanawake, kaburi wazi na kumbu kumbu endelevu ya uwepo wa Kristo Mfufuka ndicho kiini cha ujumbe wa Kesha la Pasaka 2013


Baba Mtakatifu Francisko katika Kesha la Pasaka, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekazia mambo makuu matatu: dhamana ya wanawake katika ushuhuda wa imani na upendo wao kwa Kristo; Kaburi wazi, tukio ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu na changamoto kwa waamini kuendelea kufanya kumbu kumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko, anasema, Mwijili Luka anawaonesha wanawake waliokwenda kaburini wakiwa na manukato kwa ajili ya kuupaka mwili wa Yesu. Ni kitendo cha huruma na upendo wa dhati kwa Yesu, ambaye kwa namna ya pekee, katika maisha na utume wake, aliwapatia changamoto ya kumfuasa, wakamsikiliza na kutambua kwamba, kwa hakika alikuwa ameuinua utu na heshima yao, ndiyo maana walimfuata katika Njia ya Msalaba hadi Mlimani Kalvari, wakaona mahali alipozikwa.

Kifo cha Kristo ingawa kiliacha huzuni na majonzi makubwa kwa wanawake hawa, lakini kamwe hakikuzima upendo uliowasukuma kwenda kaburini alfajiri na mapema, walipofika wakapigwa na bumbuwazi kwa kuona Kaburi wazi, jambo ambalo liliwaachia maswali magumu vichwani mwao, wakitaka kufahamu maana ya tukio hili.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, upya wa maisha unaoletwa na Mwenyezi Mungu, wakati mwingine unawaogofya wanawadamu. Kama ilivyokuwa kwa mitume wa Yesu, walijifungia katika undani wao, wakitafuta usalama na uhakika wa maisha! Kimsingi mwanadamu anaogopa kushangazwa na Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini kumwachia nafasi Mungu aweze kuwakirimia upya wa maisha.

Hii inatokana na ukweli kwamba, mara nyingi waamini wanachoka, wanakata tamaa na kuonja uzito wa dhambi zao, kiasi cha kujiuliza ikiwa kama wanaweza kweli kukabiliana na magumu pamoja na changamoto zote hizi? Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, hawajifungi katika undani wao, wala kupoteza imani na hatimaye, kukata tamaa, kwani Mwenyezi Mungu anaweza kumletea mwanadamu mabadiliko sanjari na kumsamehe dhambi zake, ikiwa kama mwamini atakimbilia huruma na upendo wake.

Mwinjili Luka anawaonesha wanawake waliokuwa wanamtafuta Yesu aliyekuwa amefufuka kati ya wafu, lakini wanaambiwa hayupo hapo amefufuka. Ufufuko wa Yesu ni tukio ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya waamini na ulimwengu kwa ujumla. Yesu Kristo amefufuka, Yu hai, anaishi kwa wakati huu na kuwaelekeza wafuasi wake kwa siku za usoni.

Huu ndio upya wa maisha unaoletwa na Mwenyezi Mungu, yaani ushindi dhidi ya dhambi na mauti pamoja na mambo yote yanayofisha utu na heshima ya binadamu, changamoto kwa waamini kuongozwa na upendo, wanapomtafuta Yesu katika hija ya maisha yao.

Matatizo na changamoto za maisha, zisiwafanye kujikuta wanatumbukia katika huzuni na simanzi kwani kwa kufanya hivi watakabiliana na kifo, kiasi cha kushindwa kumtafuta Yesu ambaye amefufuka. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumkubali na kumpokea Yesu ili aweze kuingia katika maisha yao wakimpokea kwa imani kama rafiki yao. Kama kuna mwamini aliyejisikia kuwa mbali na Yesu, akumbuke tu kwamba, Yesu bado anaendelea kufungua mikono yake kuonesha kwamba yuko tayari kumpokea kwa mikono miwili.

Kwa wale wanaoona shida na kigugumizi cha kumfuasa, wanaalikwa kupiga moyo konde kwani kwa hakika hataweza kuwalaghai, kwani daima yuko karibu na kuwakirimia amani ili waweze kuishi kama anavyotaka Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, wanawake walibahatika kukutana na upya uliokuwa umeletwa na Mwenyezi Mungu: Yesu alikuwa amefufuka na ni mzima. Baada ya kusikiliza kwa makini ujumbe juu ya Kristo Mfufuka, walioweza kuupokea kwa imani kubwa, wakikumbushwa kwamba, ilikuwa imempasa Mwana wa Adamu, kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, kusulubiwa na hatimaye siku ya tatu kufufuka kutoka katika wafu.

Changamoto kwa waamini ni kufanya kumbu kumbu endelevu ya mkutano wao na Yesu, Maneno na Matendo yake, lakini zaidi wakumbuke kwa njia ya mapendo mang'amuzi ya Kristo Mwalimu na Bwana, yaliondoa wasi wasi na woga hata wakadiriki kujitosa kimaso maso kwenda kuwapasha habari mitume juu ya ufufuko wa Kristo. Hii ni hija ya hatari anasema Baba Mtakatifu Francisko. Ni tukio linalofungua moyo ili kuweza kupokea matumaini kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi. Waamini waendelee kujifunza kumbu kumbu endelevu ambayo mwenyezi Mungu ametenda katika maisha yao,

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawakabidhi waamini chini ya maombezi ya Bikira Maria aliyebahatika kuyahifadhi matukio yote haya moyoni mwake; wamwombe Bwana yesu ili awajalie kushiriki katika Ufufuko wake, unaowakarimia waamini mabadiliko na maisha mapya. Waamini wafanye kumbu kumbu endelevu kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu anachotenda katika historia ya kila mwamini na dunia katika ujumla wake; wamwone na kujisikia kuwa yu katikati yao, daima wamtafute Yesu aliyefufuka ambaye ni mzima!







All the contents on this site are copyrighted ©.