2013-03-31 14:25:42

Ujumbe wa Papa: Urbi et Orbi kwa Mwaka 2013


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Siku kuu ya Pasaka, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tukio ambalo limehudhuriwa na umati mkubwa watu, alipanda kwenye Baraza la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ili kutoa Ujumbe na baraka zake za Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2013 kwa mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini, "Urbi et Orbi".

Baba Mtakatifu anasema, anayo furaha kubwa moyoni mwake kuwatangazia watu kwamba, Yesu Amefufuka, ujumbe unaopaswa kuingia katika kila nyumba, kila familia, lakini zaidi mahali penye mateso na mahangaiko, hospitalini na magerezani. Anapenda ujumbe huu uweze kugusa mioyo yote kwani hapa ndipo mahali ambapo Mwenyezi Mungu anapenda kupandikiza Habari Njema kwamba: Yesu Amefufuka; kuna matumaini, na wala hawako tena chini ya utumwa wa dhambi wala mateso! Ameyashinda yote haya kwa upendo na huruma!

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, ufufuko wa yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu ambao una nguvu kushinda ubaya, dhambi na kifo; ni upendo na huruma ya Mungu inayomwonjesha mwanadamu kutoka kwa Yesu Mfufuka; anayeshiriki katika utukufu wa Mungu, chemchemi ya matumaini mapya kwa binadamu.

Pasaka ni hija inayomwondoa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na ubaya na kumpatia uhuru unaofumbata upendo na wema, kwani Mungu ni uhai na utukufu wake ni mwanadamu aliye hai. Yesu ameteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu na kwamba, nguvu yake ya ufufuko ndiyo inayomwezesha mwamini kutoka katika utumwa mwa dhambi na kuelekea katika wema unaopaswa kumwilishwa katika hija ya maisha ya mwamini kila siku. Kuna majangwa makubwa ambayo mwanadamu anapaswa kuyapitia katika maisha yake!

Kubwa zaidi ni Jangwa la Moyo ambalo halina upendo kwa Mungu wala Jirani. Jangwa hili linajionesha pale mwanadamu anaposhindwa kutambua kwamba, amekabidhiwa dhamana ya kulinda na kutunza mazingira; lakini anasema Baba Mtakatifu upendo wa Mungu unaweza kuleta mabadiliko hata katika ukakasi wa maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema: kupokea neema ya Kristo Mfufuka, watoe nafasi ya kuletewa mabadiliko kwa njia ya huruma ya Mungu na upendo wa Kristo, kiasi kwamba, waweze wao wenyewe kuwa ni vyombo vya huruma ya Mungu anavyoweza kuvitumia kwa ajili ya kutunza kazi ya uumbaji na kufanya haki na amani viweshe kustawi kati ya binadamu.

Anawaomba waamini kuendelea kusali ili Yesu Mfufuka aweze kuwaletea mabadiliko ya kweli ili kutoka katika mauti na kuingia katika maisha; kuondoa chuki na kinzani kwa kupandikiza mbegu ya upendo; mahali penye kulipizana kisasi, watu wajifunze kusamehe; penye vita, amani itawale. Yesu Kristo ni amani ya watu wake na kwa njia yake, waamini wanadiriki kuombea amani kwa ajili ya ulimwengu mzima.

Baba Mtakatifu Francisiko, ameombea amani huko Mashariki ya Kati hasa zaidi kati ya Waisralei na Wapalestina, ili waweze kupata njia inayowaelekeza katika amani; wawe na ujasiri pamoja na utashi wa kuanza mchakato wa majadiliano ili kuhitimisha mgogoro ambao umedumu kwa miaka mingi. Amani nchini Iraq, kwa kusitisha vitendo vyote jinai; amani kwa Syria ambayo wananchi wake wanaendelea kuteseka kutokana na vita kuendelea kupamba moto; ongezeko kubwa la wakimbizi wanaosubiri msaada na faraja.

Damu Azizi ya Kristo imekwisha mwagika! Je, mateso kiasi gani yataendelea bado kuonekana kabla ya kupata suluhu ya kisiasa katika kinzani na migogoro hii? Anauliza Baba Mtakatifu Francisko.

Amani Barani Afrika, ambako bado vita inaendelea kupamba moto. Nchini Mali wapanie kupata umoja wa kitaifa, amani na utulivu; Nigeria ambako bado vitendo vya kigaidi vinaendelea kujirudia rudia na hivyo kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia; vitendo ambavyo kimsingi vinatishia maisha ya watu: watu wengi wametekwa nyara na vikundi vya kigaidi. Amani Mashariki mwa DRC na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambako watu wengi wamelazimika kuyakimbia makazi yao na sasa wanaishi katika hofu!

Amani Barani Asia, lakini zaidi Korea ya Kusini na Kaskazini wanakoendelea kutishiana maisha, ili waweze kuvuka tofauti zao na kuanza mchakato wa moyo wa upatanisho.

Baba Mtakafu Francisko katika ujumbe wake na baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla "Urbi et Orbi" kwa Pasaka ya Mwaka 2013 anaendelea kuombea amani duniani kote kutokana na baadhi ya watu kuelemewa na uchu wa mali, madaraka na ubinafsi; mambo yanayotishia maisha na familia ya binadamu: ubinafsi unaopelekea baadhi ya watu kujiiingiza katika biashara haramu ya binadamu; utumwa wa hali ya juu kabisa unaojionesha katika karne ya ishirini na moja.

Amani duniani katika maeneo ambayo yanashuhudia umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia kwa kutaka kuendeleza biashara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya sanjari na matumizi tenge ya rasilimali ya nchi. Amani Duniani! Yesu Mfufuka awafariji waathirika wa majanga asilia na kuwawezesha watu kuwa ni walinzi makini na wawajibikaji wa utunzaji bora wa mazingira.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wote wanaomsikiliza kwa njia ya vyombo vya upashanaji habari kutoka Roma na kutoka kila pembe ya dunia, kumwimbia Mwenyezi Mungu Zaburi kwa kusema " Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Israeli na aseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Upendo wake wadumu milele.







All the contents on this site are copyrighted ©.