Kuporomoka kwa Jengo Dar, wengi wanahofiwa kupoteza maisha!
Juhudi za kuopoa miili ya watu waliofukiwa na kifusi baada ya kuangukiwa na Jengo
la Ghorofa kumi na sita, lililoporomoka katika mtaa wa Indira Ghandhi na Barabara
ya Morogoro, Ijumaa, tarehe 29 Machi 2013 zinaendelea kwa kusua sua kutokana na ukosefu
wa vifaa vya uokoaji.
Hadi kufikia Jumamosi jioni maiti 22 zilikuwa zimeopolewa
kutoka kwenye kifusi hiki na inahofiwa kwamba, pengine kuna zaidi ya watu 60 ambao
wamefariki dunia baada ya kuangukiwa jengo hili ambalo kwa sasa linafanyiwa uchunguzi
na vyombo vya usalama ili kubaini chanzo chake nini!
Wahandisi na Makandarasi
wanapaswa kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, maadili na weledi ili kupunguza
kama si kusitisha kabisa ajali kazini. Fedha ikitangulizwa mbele na kubeza maisha
na utu wa mwanadamu, kuna hatari kubwa ya majengo kama haya kuendelea kuporomoka,
kama hofu inayoendelea kutanda kwa jengo pacha karibu kabisa na mahali ambapo ajali
hii imetokea.