2013-03-30 15:11:47

Sanda takatifu ni kielelezo cha hali ya juu cha huruma na upendo wa Mungu uliomwilishwa katika historia


Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, katika Ibada ya Kuabudu Sanda Takatifu ya Yesu. Anasema, kwa njia ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, leo hii waamini wanaweza kushiriki katika tukio hili la imani. Hata katika mazingira kama haya anasema, Baba Mtakatifu Francisko, waamini hawaweze kusimama hivi hivi tu, bali wanapaswa kuonesha heshima na ibada.

Hii ni Sanda inayoonesha uso wa mtu aliyefariki dunia, lakini bado anaendelea kuwatazama waja wake katika hali ya ukimya na kutoka katika undani wao, anaweza tena kuzungumza nao! Ni Jambo la ajabu kuona kwamba, waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wamekwisha kupata fursa ya kusimama na kufanya tafakari ya kina kuhusu Mtu huyu alisulubiwa na kufa juu ya Msalaba.

Sanda Takatifu ni mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu Yesu wa Nazareti. Sura iliyochapwa kwenye Sanda Takatifu ni mwaliko kwa waamini kukwea kwenda Mlimani Kalvari, ili kuutafakari Mti wa Msalaba, unaoonesha katika ukimya fadhila ya upendo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiruhusu ili waguswe na macho yanayopenda kutoka katika Sanda Takatifu. Katika hali ya ukimya, wasikilize kwa makini yale ambayo Yesu anataka kuwashirikisha nje ya kifo chake. Sanda hii ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu uliofanyika Neno; Na Neno akafanya Mtu na kuzaliwa katika historia, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, kiasi kwamba, aliweza kujitwalia juu yake maovu na dhambi za binadamu, ili aweze kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Uso unaoonekana kwenye Sanda Takatifu wa mtu ambaye amekabiliwa na mateso makali ni kielelezo makini cha wale wote ambao utu na heshima yao havithaminiwi tena; wanaendelea kukabiliana na vita na uvunjifu wa haki msingi za binadamu bila kusahau mateso ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ni Uso unaoonesha pia amani na utulivu wa ndani wa mtu ambaye kwa hakika alikuwa na ujasiri mkubwa, changamoto ya kuendelea kuimarisha imani bila kupoteza matumaini na upendo wa Mungu, ili nguvu ya Kristo mfufuka iweze kuyashinda yote.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari hii, mbele ya Sanda Takatifu, anapenda kusali kwa kutumia maneno ya Mtakatifu Francisiko wa Assisi aliyosali mbele ya Msalaba akimwomba Mwenyezi Mungu aweze kuliangazia giza la moyo wake, amkirimie imani thabiti, matumaini na mapendo ya kweli; aweze kuwa na upeo wa kuelewa ili hatimaye, aweze kutekeleza kwa dhati kabisa ile amri ya upendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.