2013-03-30 15:09:21

Sanda Takatifu inaonesha imani na nguvu ya upendo wa Mungu kwa binadamu


Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, Italia katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2013, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kulijalia Kanisa kumpata Mchungaji Mkuu, Baba Mtakatifu Francisko, anayechomoza kama miali ya jua la alfajiri.

Papa amepokelewa na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa mikonomiwili, alama ya Pasaka Mpya katika Kanisa, inayotolewa na Kristo mwenyewe kwa kulipatia Kanisa lake na ulimwengu kwa ujumla, nguvu na ujasiri wenye matumaini. Huu ni mwaliko na changamoto ya kutolea ushuhuda wa imani tendaji, kwa kupokea na kukumbatia Msalaba unaokoa; chemchemi ya wokovu na upendo wa Mungu, unaopaswa kupelekwa kwa maskini na wanyonge ndani ya Jamii.

Waamini wanahamasishwa kulinda na kutunza mazingira; kujenga na kuimarisha umoja, udugu na mshikamano wa dhati kwa kuondokana na kinzani na vikwazo vinavyopelekea migawanyiko katika Jamii. Baba Mtakatifu Francisko, tangu kuchaguliwa kwake, ameonesha kuwa ni mtu wa watu na kwa ajili ya watu, ili kuweza kuwaonesha ile njia inayokwenda kwa Kristo.

Ameonesha na kushuhudia kwa njia ya maisha na utume wake, maana ya uongozi kuwa ni kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wanyonge na maskini. Kwa muda mfupi, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuwashirikisha ndugu zake katika Kristo fadhila na utajiri wake wa imani na mapungufu yake ya kibinadamu.

Mwaka huu, wakati wa Jumamosi kuu, Sanda Takatifu imeoneshwa kwa njia ya Luninga, kutoka katika Kanisa kuu la Jimbo kuu la Torino, tukio ambalo waamini na watu wenye mapenzi mema wamelifuatilia kwa unyenyekevu mkubwa kwa kuona ile nguvu ya upendo wa Mungu unaojionesha kwa njia ya Sadaka ya Yesu Kristo pale Msalabani.

Ndani ya Kanisa kuna watu wanaobeba Misalaba ya maisha, alama makini ya mateso ya Kristo, changamoto kwa waamini hawa kuuishi Msalaba wao kwa Imani, wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, daima wakiwa tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya jirani zao!

Sanda Takatifu inaonesha kwamba, kupenda maana yake ni kuteseka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo, Kanisa na mafao ya wengi, kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu unashinda maovu ya dunia hii na kwamba, mema yanaweza kuleta mabadiliko ya pekee katika maisha ya mwanadamu kuelekea katika safari ya ukombozi.

Sanda Takatifu inayooneshwa Jumamosi Kuu inamwonesha Kristo Msulubiwa, Imani na nguvu ya Upendo wa Mungu unaomwezesha mwanadamu kufufuka kutoka katika wafu; kuonja matumaini ya ushindi wa Mungu dhidi ya dhambi na mauti kwa njia ya Yesu Kristo Mfufuka. Ni changamoto kwa waamini kukumbatia msamaha dhidi ya chuki na uhasama na kuendelea kujikita zaidi katika maisha, sala na upendo, kiasi hata cha kuonesha upendo huu katika wito wa maisha ya Kipadre, Kitawa na Ndoa Takatifu.

Ni changamoto ya kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu; kutafuta kwanza kabisa mafao ya wengi; daima haki, amani, upendo na mshikamano vikipewa msukumo wa pekee. Kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapaswa kupokelewa, kuthaminiwa na kupendwa bila kubezwa wala kutezwa kutokana na hali yake ya maisha; kama kilema, mgonjwa, mhamiaji au mtu aliyesukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kipindi cha Pasaka kiwe ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, kila mwamini ajitahidi kuwa chembe chembe ya matumaini katika ulimwengu mamboleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.