Salam za kheri na matashi mema kwa Papa Francisko kwa Siku kuu ya Pasaka 2013
Rais Giorgio Napolitano wa Italia amemwandikia salam za kheri na baraka Baba Mtakatifu
Francisko wakati huu anapoadhimisha Siku kuu ya Pasaka kwa mara ya kwanza kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Kwa niaba yake mwenyewe na wananchi wa Italia katika ujumla wao,
anachukua fursa hii kumtakia Baba Mtakatifu Francisko mafanikio mema katika maisha
na utume wake.
Rais Napolitano anasema, Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa
Mwaka huu yanafanyika wakati nchi ya Italia ikiwa inakabiliana na changamoto kubwa
za mabadiliko katika mfumo wake wa demokrasia na uongozi wa ngazi za juu katika mihimili
mikuu ya uongozi kitaifa.
Hii ni changamoto ya kujenga utamaduni wa kusikiliza
na kutoa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya amani, haki na mshikamano pamoja
na kutafuta nguvu inayohitajika ili kuweza kupokea ujumbe wa Kikristo na ule wa jumla
unaopania kuwa ni mwanzo mpya sanjari na kuwajengea watu matumaini mapya yanayoendelea
kujionesha sehemu mbali mbali za dunia.
Rais Giorgio Napolitano anahitimisha
salam na ujumbe wa matashi mema ya Pasaka kwa Baba Mtakatifu Francisko, huku akimwahakikishia
urafiki na ushirikiano anapotekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.