2013-03-30 07:46:24

MSALABA ni kielelezo cha: Upendo, huruma, msamaha na hukumu!


Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza, tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameshiriki katika Ibada ya Njia ya Msalaba, iliyofanyika kuzunguka magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, tarehe 29 Machi 2013, Usiku, ibada ambayo imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Mara baada ya ibada ya Njia ya Msalaba, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wale wote waliohudhuria Ibada hii sanjari na wote waliokuwa wanaifuatilia kwa njia za mwasiliano ya Jamii. Kwa namna ya pekee, amewakumbuka wagonjwa na wazee, wanaoendelea kuibeba Misalaba katika hija ya maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu anasema, MSALABA unapaswa kuwa ndiyo neno msingi katika maadhimisho ya Njia ya Msalaba.

Msalaba ni jibu makini ambalo Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo amelitoa kwa walimwengu dhidi ya dhambi. Wakati mwingine Mwenyezi Mungu anaamua kukaa kimya, lakini hata katika ukimya huu, bado anaendelea kuzungumza na kujibu kilio cha waja wake kwa njia ya Fumbo la Msalaba.

Baba Mtakatifu anasema Msalaba unafumbata kwa namna ya pekee: upendo, huruma, msamaha na hukumu. Mwenyezi Mungu anamhukumu mwanadamu kwa kumwonjesha upendo, ikiwa kama mwanadamu ataweza kulipokea pendo hili, atapata uzima wa milele, lakini akilitema, kwa hakika atakuwa amejihukumu mwenyewe, kwani kimsingi Mwenyezi Mungu anapenda na kuokoa.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Msalaba ni jibu makini kwa Wakristo dhidi ya magumu yanayowaandama na kuwazunguka katika hija ya maisha na utume wao, changamoto kwa waamini kujibu ubaya kwa kutenda wema, kwa kujitwika Msalaba kama alivyofanya Kristo mwenyewe. Itakumbukwa kwamba, Taafakari ya Njia ya Msalaba na Sala kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2013 imetayarishwa na vijana wawili kutoka Lebanon na kuhaririwa na Kardinali Butros Becharà Rai, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti wa Lebanoni.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru wote waliohusika kwa ushuhuda huu makini, kumbu kumbu endelevu ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita nchini Lebanon. Tafakari hii imeonesha na kugusa ile nguvu ya ushuhuda wa umoja wa Wakristo katika Nchi Takatifu; urafiki na udugu miongoni mwa Wakristo, Waislam na Waamini wa dini nyingine. Tukio hili ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Nchi za Mashariki ya Kati na Ulimwengu kwa ujumla.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anawaalika waamini kuendeleza Njia ya Msalaba katika maisha ya kila siku. Anawaalika kutembea katika Njia ya Msalaba, wakibeba ndani mwao upendo na msamaha; wakiwa na matumaini katika ufufuko wa Kristo, aliyewapenda upeo na kwamba, kila kitu ni upendo!

Umati mkubwa wa watu ulizunguka magofu ya Colosseo, wakati ambapo Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma alipokuwa anaongoza Ibada ya Njia ya Msalaba, iliyokuwa na uwakilishi mzito kutoka: Lebanon, Italia, India, China, Nchi Takatifu, Afrika na Brazil. Mara baada ya Ibada ya Njia ya Msalaba, Kwaya ya Makleri kutoka Lebanon, iliimba. Kwa hakika, tafakari na sala ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2013 ilikuwa na ujumbe mzito!







All the contents on this site are copyrighted ©.