Kukamatwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya Padre Evaristi Mushi, Jimboni Zanzibar uwe ni
mwanzo wa kufahamu nani anahusika na chokochoko za kidini Tanzania!
Maafisa wa Upepelezi wa Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na na Makachero
wa Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI, kwa pamoja wamefanikiwa kumtia pingu Omar
Mussa Makame (35) anayetuhumiwa kumuua kwa kumpiga risasi Padre Evarist Mushi wa Jimbo
Katoliki Zanzibar, kunako tarehe 17 Februari 2013.
Hayo yamebainishwa na Kamishina
wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa na kwamba, hatua zaidi za kisheria zimekwishachukuliwa
na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani mapema iwezekanavyo.
Wachunguzi
wa masuala ya haki msingi za binadamu, utawala wa sheria na uhuru wa kuabudu wanasema,
hii ni hatua ya kwanza katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, sheria inashika mkondo
wake. Lakini jambo la msingi ambalo watanzania kwa sasa wanataka kulifahamu ni nani
anayehusika na choko choko za kidini ambazo kwa sasa zimewajengea watanzania wengi
hofu hata ya kuanza kuogopa kwenda Makanisani kusali?
Changamoto kwa wakati
huu ni kuendeleza majadiliano ya kidini ili haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa
viweze kutawala tena na kamwe watanzania wasikubali kutumiwa na baadhi ya watu wanaotaka
kuvuruga amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kwa mafao yao wenyewe!