Kesha la Pasaka ni Usiku Mtakatifu ambao Mama Kanisa amekuwa akiuadhimisha kwa heshima
kuu kadiri ya Mapokeo yake. Ni Usiku wenye utajiri mkuu wa maisha ya kiroho, mwaliko
kwa waamini kuendelea kukesha huku wakisubiri ujio wa pili wa Yesu Kristo, atakapokuja
kuwahukumu wazima na wafu na kwamba, ufalme wake hauna mwisho. Usiku wa Pasaka ni
kielelezo cha waamini kuvuka kutoka katika dhambi na mauti na kuanza hija ya maisha
mapya katika Kristo Mfufuka. Katika Kesha la Pasaka, Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo
cha Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti, ndiyo maana Mama Kanisa anathubutu
kuimba sifa za Mshumaa wa Pasaka “Exultet” Yaani Mbiu ya Pasaka. Ni kesha lenye utajiri
mkubwa wa Liturujia ya Neno la Mungu, inayowakumbusha waamini mchakato wa historia
ya ukombozi wa mwanadamu, tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi Siku ya kwanza ya Juma,
Yesu Kristo alipofufuka kutoka katika wafu, mwaliko wa kuwashirikisha waamini katika
Fumbo la Pasaka kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na kwa wale waliokwisha kubatizwa
basi, wanapata nafasi ya kurudia tena ahadi zao za ubatizo. Baba Mtakatifu Francisko,
katika Kesha la Pasaka, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, anatarajiwa
kutoa Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu kwa Wakatekumeni kutoka
Italia, Albania, Russia na Marekani. Wakristo hawa wapya wataungama imani na kushiriki
katika Sala ya kuliombea Kanisa, sala ambayo inajulikana na wengi kuwa ni Sala ya
Waamini. Mwishoni, Waamini wanaadhimisha Liturujia ya Ekaristi Takatifu, ambamo
Yesu Kristo, Mwanakondoo aliyeteswa, akafa na kufufuka anajitoa tena kuwa ni Ekaristi,
chakula na kinywaji cha kiroho, changamoto kwa kila mwamini kuwa ni Ekaristi Takatifu
kwa jirani yake, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana
na hali n anafasi yao katika maisha. Kwa namna ya pekee, waamini wanaoshiriki Ekaristi
Takatifu, wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka
kwa njia ya utakatifu wa maisha. Kesha la Pasaka anasema Mshehereshaji mkuu wa
Ibada za Kipapa, Monsinyo Guido Marini ni kilele cha Maadhimisho ya Siku tatu za Mafumbo
ya Ukombozi, yaani Alhamisi kuu, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja
Takatifu na kuhimiza huduma ya upendo na mshikamano wa dhati. Ijumaa kuu, Kanisa limefanya
kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo. Siku kuu ya Pasaka ni chemchemi ya furaha
na matumaini inayopata mwendelezo wake katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.