Jumuiya ya Kimataifa yashindwa kufikia muafaka kuhusu udhibiti wa biashara ya silaha
duniani!
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon ameonesha masikitiko yake makubwa
baada ya wajumbe wa mkutano wa Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili kuhusu mkataba
wa biashara ya siilaha kimataifa kuhitimishwa mwishoni mwa juma, bila kufikia muafaka.
Wajumbe kutoka Korea ya Kaskazini, Iran na Syria, baada ya majadiliano kwa
takribani majuma mawili waliamua kupinga mkataba huu na hivyo Jumuiya ya Kimataifa
ikajikuta inakwama katika utekelezaji wake.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
anabainisha kwamba, Mkataba huu ni muhimu sana na umeandikwa kwa ufasaha kwa kuangalia
mahitaji ya Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Ni matumaini ya Katibu mkuu wa Umoja
wa Mataifa kwamba, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, watajipanga kwa mara nyingine,
ili kuweza kuupitisha Mkataba huu kwa kupigiwa kura na wajumbe wapatao theluthi mbili.
Wajumbe
wengi walianza kuonesha matumaini ya Mkataba huu kuweza kupitishwa na hivyo kuwa ni
tukio la kihistoria, baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kutoa changamoto kubwa
katika udhibiti wa silaha nchini Marekani. Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, waathirika
wakuu wa biashara ya silaha kimataifa ni watu wanaoishi Barani Afrika na Amerika ya
Kusini.
Wakati wa ufunguzi wa mkutano huu hapo tarehe 18 Machi 2013, Wajumbe
kutoka Barani Afrika walikuwa wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuweka viwango vya hali
ya juu kimataifa, ili kukomesha biashara haramu ya silaha kimataifa, ambayo imekuwa
ni chanzo cha vita, kinzani na vurugu za kijamii Barani Afrika na sehemu nyingine
za dunia.
Akichangia mada katika mkutano huu, Rais Ellen Jonhson Sirleaf wa
Liberia ambaye pia ni mshindi wa tuzo la amani, amesema kwamba, kuna mamillioni ya
watu wanaendelea kupoteza maisha na wengine wengi kupata majeraha na ulemavu wa kudumu
kutokana na kuzagaa kwa silaha za moto!