Njia ya Msalaba: daraja linalowavusha watu kutoka katika mauti ili kupata maisha mapya!
Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo iliyoandaliwa na Vijana kutoka
Lebanon na kuhaririwa na Kardinali Bèchara Boutros Rai, Patriaki wa Kanisa la Maroniti
la Antiokia. Ni mwaliko kwa
wafuasi wa Kristo kutumia Msalaba kama daraja linalomvusha mwanadamu kutoka katika
kifo kuelekea maisha ya uzima wa milele. Ni changamoto kwa vijana na wote wanaokumbana
na kinzani, migogoro na migawanyiko ya kikabila, kidini na kijamii; wanaokabiliana
na vita na ukosefu wa haki msingi; vijana wanatakiwa na Mama Kanisa kuwa ni alama
ya matumaini na wajenzi wa amani. Hata leo hii mchakato wa kumhukumu Yesu bado
unaendelea kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya watu wanapenda kumng’oa Mungu
kutoka katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu. Kuna baadhi ya watu wanaotaka kufisha
tunu za imani, utu na maadili mema kwa kisingizio cha kutaka kulinda na kudumisha
demokrasia na uhuru wa kuabudu. Watu wanaoteseka na kudhulumiwa hasa walioko Mashariki
ya Kati wauone Msalaba kama alama ya matumaini, ili hatimaye, waweze kuona ukweli
na kuonja upendo. Yesu bado anawaalika waamini kusimama na kuendelea mbele na hija
ya maisha yao ya kiroho hata baada ya kuanguka, kusimama na kuendelea na safari ya
kuutafuta ukweli kwa kutumia vyema imani na akili yake, ili kweli aweze kupata utimilifu
wa ukweli wote. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni mfano bora wa kuigwa. Ni
Tabernakulo ya kwanza ya Neno la Mungu; ni mwanfunzi makini aliyejifunza kufanya tafakari
ya kina katika ukimya, akabahatika kukutana naye katika Njia ya Msalaba. Hata leo
hii, bado wazazi wengi wanaendelea kuteseka kutokana na mateso ambayo wazazi wanawapatia
watoto wao au watoto wanawafanyia wazazi wao. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba,
Familia za Kikristo zinakuwa ni mahali muafaka pa kukutana na kuonesha uwapo endelevu
wa Yesu katika hija ya maisha ya watu wake; daima wakijitahidi kuiga mfano wa Familia
Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kila mtu ana Msalaba wake, lakini katika yote
haya, waamini wanapaswa kujifunza kukubali na kuipokea Misalaba ya maisha yao kwa
imani, mapendo na matumaini; wakiendelea kuwa na dhamiri hai, wakisikiliza kwa makini,
wakiwa na kiu ya kutaka kufahamu ukweli pamoja na kutumia vyema uhuru wao wa kuabudu. Waamini
katika hija ya maisha yao hapa duniani wanautafuta Uso wa Yesu, changamoto kwa waamini
na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu,
utu na heshima ya wote, hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na umaskini,
ujinga na maradhi. Yesu anapoanguka mara ya pili, anawachangamotisha waamini na
watu wote wenye mapenzi mema, kuangalia kinzani na migogoro ya kidini inayoendelea
kufuka moshi sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa kuwa na dhamiri nyofu, waoneshe
utashi wa majadiliano ya kidini na ushirikiano wa dhati licha ya tofauti zao za kiimani.
Kwa pamoja wasimame kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu, maendeleo, mafao na
ustawi wa wote. Katika mahangaiko yote haya, waamini wanaalikwa kutolea ushuhuda wa
imani na upendo wa Kristo kwa wote. Waamini wanakumbushwa kwamba, dunia ya leo
imesheheni wanawake wanaodhulumiwa na kunyanyaswa utu na heshima yao, wanaobaguliwa
na kutengwa. Wote hawa Kristo awe ni amani yao. Bikira Maria aliyebahatika kuwa ni
Tabernakulo ya Fumbo la Umwilisho, ameuinua utu na heshima ya kila mwanamke. Yesu
awe kweli ni faraja ya wanawake wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Yesu
anapoanguka mara ya tatu, anawakumbusha waamini kwamba, uzito wa dhambi za binadamu
unamwelemea. Anamwonesha binadamu kwamba, hata katika udhaifu wake bado anaweza kushinda
magumu na vishawishi akaamka na kusonga mbele, kwa kuchota neema na baraka kutoka
katika Sakramenti za Kanisa; ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa; Umoja na
Mshikamano wa dhati; upendo na unyenyekevu. Msalaba wa Kristo uwe ni daraja linalowaunganisha
waamini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Kuna watu sehemu mbali mbali
za dunia wanaendelea kuvuliwa utu na heshima yao kutokana na madhulumu kiasi cha kukimbia
hata makazi yao wenyewe. Wote hawa wawe na ujasiri wa kubaki katika maeneo yao, ili
kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima
yuko kati yao! Yesu aliyefungwa mikono na miguu pale Msalabani kwa njia ya misumari
aendelee kuwaombea binadamu wote, ili kwa jicho lake la upendo kutoka pale Msalabani,
aweze kuwaponya wagonjwa na kuwasamehe wadhambi na upendo wake uweze kuifunika dunia
yote. Kanisa linawaombea vijana wanaokata tamaa kiasi cha kujikuta wakitumbukia katika
matumizi haramu ya dawa za kulevya; wakijiingiza katika madhehebu na anasa, ili waonje
upendo na kupata furaha ya kweli kutoka kwa Kristo. Yesu anapokufa pale Msalabani,
Kanisa linayaelekeza macho yake kwa wale wote wanaokumbatia utamaduni wa kifo, kutubu
na kuongoka, ili waweze kuuona ukweli na wajenzi wa utamaduni wa upendo na watangazaji
hodari wa Injili ya Uhai. Yesu anapozikwa Kaburini, hapo baadhi ya watu wanadhani
kwamba, ubaya na dhambi vimeshinda na kwamba: sauti ya ukweli, upendo, haki na amani
haina nafasi tena. Vitendo vya kigaidi, mauaji, chuki na hali ya kulipizana kisasi
vinaonekana kushamiri. Kanisa linachukua nafasi hii kwa ajili ya kuwaombea waathirika
wa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, wakimbizi na watu wasiokuwa na
makazi waweze kurejea tena katika makazi yao; damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea
kumwagika iwe ni mbegu ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, ili dunia
iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kukazia na kudumisha tunu msingi
za kitamaduni, maisha ya kiroho na kiutu. Mbele ya kifo, mateso na machungu ya
maisha, hapa kunahitajika matumaini nai mani thabiti. Mateso, kifo na ufufuko wa Yesu
ni changamoto ya kutembea katika mwanga wa maisha mapya, kwa kuonesha umuhimu wa zawadi
ya maisha, kwa wale wote waliokata tamaa ya maisha, kwani Kanisa lina amini katika
ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti.