Imani ya Kanisa imesimikwa katika Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka!
Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anaendelea
kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato
wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuweza kulinda na kudumisha misingi ya
haki, amani, upendo, udugu na upatanisho wa kweli, kama alivyofanya Mtakatifu Francisko
wa Assisi enzi ya uhai wake.
Alipinga vita
vya kidini na kutaka waamini kujenga utamaduni wa upatanisho kama njia ya kuimarisha
amani na uelewano kati ya watu wa dini mbali mbali na kwamba, tofauti zao za kiimani,
kisiwe ni kisingizio cha kuleta vita na machafuko miongoni mwa Jamii.
Kardinali
Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar
ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika mahojiano na Radio
Vatican anabainisha kwamba, Kanisa linamwamini Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka
kutoka katika wafu, changamoto ya kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa
kweli, kwani kwa njia ya Damu yake Azizi, ameukomboa ulimwengu na kumpatanisha mwanadamu
na Muumba wake.
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunza kwamba, sera ya vita
na matumizi ya nguvu zimepitwa na wakati na matokeo yake ni watu wasiokuwa na hatia
kuendelea kupoteza maisha yao, badala yake, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujikita
katika majadiliano ya kina, ili haki, amani na upatanisho viweze kustawi na kushamiri
tena miongoni mwa Jamii.
Kardinali Pengo katika mahojiano na Radio Vatican
amegusia pia chokochoko za kidini zinazoendelea kushika kasi nchini Tanzania. Wito
wake ambao ameendelea kukazia wakati wote ni kuwataka Wakristo na watanzania wenye
mapenzi mema, kujikita katika mchakato wa kutafuta misingi ya haki na amani kwa njia
ya majadiliano ya kina yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na upendo miongoni mwa Jamii,
daima wote wakipania kutafuta: ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, kwani amani ni
jina jingine la maendeleo.
Kardinali Pengo anawakumbusha Wakristo kwamba, wanamfuata
Kiongozi wao ambaye ni Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu
ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia hii akawashirikisha
wafuasi wake katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika amani. Hiki ni kielelezo
kwamba, Kristo anawatakia amani wafuasi wake; amani ambayo wanapaswa pia kuwashirikisha
wengine katika hija ya maisha yao!
Kuchukua silaha na kuanza mapambano ni kinyume
cha mafundisho ya Kristo na kamwe Wakristo wajishikwe na kishawishi cha kutaka kulipiza
kisasi, kwani Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkirimia mwanadamu amani
ya kweli. Ni changamoto ya kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini; kwa kuheshimiana
na kuthaminiana kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.