2013-03-28 08:19:56

Wananchi wa Cuba kwa mara ya kwanza wanaadhimisha Ijumaa Kuu kama Siku ya Mapumziko Kitaifa


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Cuba, Mwaka huu, Wakristo wataweza kuadhimisha Ijumaa kuu, siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka kwa namna ya pekee, mateso na kifo cha Kristo Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, kama Siku ya Mapumziko Kitaifa. RealAudioMP3

Uamuzi huu umetolewa hivi karibuni na Serikali ya Cuba kama sehemu ya kumbu kumbu ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita nchini Cuba.

Taarifa ya Shirika la Habari za Kanisa Zenit inabainisha kwamba, kunako mwaka 1998 mara tu baada ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kutembelea nchini Cuba kwa mara ya kwanza, Siku kuu ya Noeli, ikatangazwa kuwa ni Siku ya Mapumziko Kitaifa, mwaka mmoja baada ya hija hii ya kihistoria kufanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro nchini Cuba.

Hata habari za Ijumaa kuu kuwa ni Siku ya Mapumziko Kitaifa nchini Cuba, imetolewa mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alipotembelea nchini Cuba. Lakini kwa namna ya pekee, uamuzi huu umetangazwa wakati ambapo Baba Mtakatifu Francisko anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo makini cha utashi wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa nchini Cuba.

Hizi ni dalili njema za maboresho ya uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Cuba, ambao kwa takribani miaka 50 ulikuwa ni wavuta nikuvute! Ni kipindi ambacho kilisheheni ukanimungu na Siku kuu muhimu katika maisha na utume wa Kanisa kama vile Ijumaa kuu na Pasaka zikafutwa kutoka kwenye Kalenda ya Cuba.

Kunako mwaka 1961, Kanisa likapigwa rufuku ya kutumia vyombo vya mawasiliano ya Jamii na baadhi ya mali zake zikataifishwa. Lakini, katika miaka ya hivi karibuni, pole pole, Serikali imeanza kuonesha ushirikiano wa karibu zaidi na Kanisa kwa kutoa vibali vya ujenzi na ukarabati wa Makanisa kutokana na fedha za misaada zinazotolewa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa na kidini wanabainisha kwamba, mabadiliko makubwa nchini Cuba yalianza kuonesha cheche zake kunako mwaka 1993. Wakristo wakaruhusiwa kuhudhuria Ibada mbali mbali. Serikali ikatambua na kuthamini utume na huduma zilizokuwa zinatolewa na Kanisa nchini Cuba.

Parokia zikawa ni mahali pa majiundo makini ya waamini nchini humo kiasi kwamba, Kanisa likapewa dhamana ya kuwahudumia kiroho wafungwa waliokuwa magerezani. Watawa na Mapadre waliokuwa wanatoa huduma ya upendo Hospitalini wakaruhusiwa kuendelea na utume wao. Vyombo vya mawasiliano nchini Cuba vinamilikiwa na kuendeshwa na Serikali, lakini Maaskofu wanaruhusiwa kuvitumia kwa ajili ya kuzungumza na waamini wao! Haya ni matendo makuu ya Mungu katika historia ya wananchi wa Cuba.

Itakumbukwa kwamba, tangu ulipoanza mchakato wa kumtafuta Papa Mpya kwa mikutano elekezi ya Makardinali mjini Vatican, wananchi wa Cuba walipara fursa ya kuweza kufuatilia matukio haya moja kwa moja yakirushwa kutoka mjini Vatican, jambo ambalo lingekuwa ndoto miaka kadhaa iliyopita. Baadhi ya sehemu za Ibada ya mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu wa Roma, zilitangazwa tena na vyombo vya habari nchini Cuba. Kwa hakika, Kanisa ni mdau mkubwa wa maendeleo na wala si mpinzani kama wanavyodhani baadhi ya wanasiasa!








All the contents on this site are copyrighted ©.