2013-03-28 12:47:13

Papa Francisko aadhimisha Ibada ya Kubariki Mafuta Matakatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican


Kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu, tarehe 28 Machi 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta Matakatifu pamoja na Makleri wanaotekeleza utume wao katika Jimbo kuu la Roma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Katika Ibada hii, amebariki mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa na Krisma ya Wokovu. Mapadre pia wamerudia ahadi za utii kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewapongeza kwa namna ya pekee, Makleri wanaoadhimisha kumbu kumbu ya siku ile walipopewa Daraja Takatifu. Ni makuhani waliopakwa mafuta kama inavyosimuliwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu, ili kuwatangazia Maskini Habari Njema ya Wokovu. Anasema, mavazi ya Liturujia yana alama makini zinazodhihirisha dhamana na utume wa Makleri wanapoadhimisha Mafumbo ya Kanisa.

Wanaalikwa kwa namna ya pekee, kuwabeba mabegani mwao watu ambao wamedhaminishwa kwao na Mama Kanisa na kwamba, majina yao yameandikwa kwenye mioyo yao. Mavazi ya Kikasisi ni changamoto kwa Mapadre kusikia uzito wa Waamini, Watakatifu na Mashahidi. Liturujia anasema Baba Mtakatifu Francis inaonesha ule mng'ao wa utukufu wa Mungu. Mafuta matakatifu yanalenga kuganga madonda ya Maskini, Wagonjwa, Wafungwa, Pweke na wale wote wanaoogelea katika dimbwi la huzuni.

Ni wajibu wa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanawapaka mafuta ya furaha na matumaini waamini wanaohudhuria Ibada kwa kuwatangazia Habari Njema inayogusa undani wa maisha yao ya kila siku. Mafuta haya yawalinde waamini wanaoishi pembezoni mwa Jamii, ambao daima imani yao iko hatarini, kwa kushiriki katika furaha, matumaini na mahangaiko yao ya ndani, kiasi kwamba, wanakuwa tayari kuomba huruma na upendo wa Kristo katika shida na mahangaiko yao. Mapadre wanapodumisha uhusiano wao wa dhati na Mwenyezi Mungu wanakuwa ni daraja la neema na baraka kati ya Mungu na waamini wao.

Mapadre wawe ni chemchemi ya neema kwa watu wao, kama ilivyokuwa kwa wakati wa Yesu, wagonjwa na wenye shida walipotamani walau kugusa hata pindo la mavazi yake; hiki ni kielelezo cha imani inayojificha katika mahangaiko ya watu mbali mbali, changamoto ya kwa Mapadre kuzama katika undani wa mambo badala ya kuangalia na kuchukulia mambo juu juu tu, kama ilivyotokea pale yule Mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa miaka minane alipogusa vazi la Yesu na kupona ugonjwa wake.

Katika tukio hili, Mitume wa Yesu waliona umati mkubwa wa watu uliokuwa unamzonga zonga Yesu! Lakini Yesu aliiona imani ya yule Mwanamke. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ndiyo changamoto kwa Makleri kutekeleza wajibu na utume wao mahali penye shida: pale ambapo damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika bure! Mahali ambapo vipofu wanatamani kuona.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, watu wanaguswa na neema iliyoko ndani mwao ili waweze kukua na kukomaa katika imani. Kwa njia hii, Makleri wataweza kuwatangazia Injili wengine pamoja na kuwashirikisha kile kidogo walichonacho wale ambao hawana kitu kabisa!

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre kwamba, wasipojitoa katika ubinafsi wao, hawataweza kushirikisha utajiri mkubwa unaofumbatwa katika mioyo na utumishi wao. Watashindwa kuwa kweli ni kiungo na daraja kati ya Mungu na watu na badala yake watakuwa ni watawala na watu wa mshahara; watu ambao kamwe hawawezi kujitoa kimasomaso, hawataweza kupokea moyo wa shukrani na matokeo yake ni kukata tamaa na kuanza kugubikwa na huzuni badala ya kuwa kweli ni wachungaji wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kondoo wao. Watambue kwamba, wao kimsingi ni wavuvi wa watu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ukosefu wa utambulisho wa uhakika wa wito na maisha ya Kipadre ni hatari kwa Makleri wote kwani huu ni myumbo wa utamaduni, lakini Makleri hawana sababu ya kuogopa kwani wakiwa na imani thabiti, wanaweza kutweka hadi kilindini, hali wakionesha ule utambulisho wao kama wapakwa mafuta wa Bwana. Huu ni mwaliko wa kushirikiana na Yesu, Kuhani mkuu.

Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini kuwa karibu zaidi na Mapadre wao kwa njia ya mapendo, lakini zaidi katika huduma na sala, ili daima waendelee kuwa ni wachungaji wema kadiri ya mapenzi ya Mungu. Amewaombea Mapadre ili waweze kuwa na moyo wenye utakatifu wa maisha, utakaowasukuma hadi pembezoni mwa Jamii, mahali ambapo waamini wanawasubiri kwa ari na moyo mkuu.

Mapadre wajitahidi kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo, utambulisho wao unaojionesha kwa namna ya pekee katika matendo. Kwa njia ya Mapadre ambao wamepakwa mafuta, waamini waweze kuonja furaha ya kweli iliyoletwa na Yesu Kristo mpakwa wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko amefanya kumbu kumbu ya miaka 44 tangu alipopewa Daraja Takatifu la Upadre.







All the contents on this site are copyrighted ©.