2013-03-28 08:39:19

Maisha ya Mapadre yawe ni kielelezo cha Fumbo la Imani wanalolitangaza na kuliadhimisha!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kama sehemu ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki. RealAudioMP3

Kardinali Pengo anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu la Upadre. Katika Fumbo la Ekaristi, Mapadre wanatangaza Fumbo la Imani, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ekaristi Takatifu ni kielelezo endelevu cha uwepo wa Kristo miongoni mwa wafuasi wake kwa njia ya Maumbo ya Mkate na Divai. Kristo nduye Kuhani mkuu aliyejinyenyekesha, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu.

Mapadre wanaadhimisha Fumbo hili la Imani kwa niaba ya Yesu Kristo, changamoto kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, maisha na matendo yao yanamfanana Kristo. Kwa namna ya pekee, Mapadre wanaalikwa kuliishi Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kujitoa kikamilifu kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake, kwa kuendelea kuwaimarisha waamini katika imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili, kielelezo cha hali na maisha ya ndani.

Mapadre wanapotangaza Fumbo la Imani, wanahusishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kristo, kiasi kwamba, wanakuwa ni Kristo wengine. Huu ni mwaliko anasema Kardinali Pengo kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, maisha yao yanalingana na Fumbo wanaloadhimisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.