2013-03-27 08:07:24

Vijana wajibikeni kikamilifu katika maisha ya kiraia, kijamii na kiroho!


Askofu Gevas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, Tanzania katika Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi sanjari na Siku ya Vijana Kijimbo, amewataka vijana nchini Tanzania kuwajibika kikamilifu katika maisha ya Kijamii na Kiroho kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kama vijana, lakini zaidi kama watanzania. RealAudioMP3

Juma kuu ni kipindi maalum kinachotoa fursa kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu Mafumbo ya Ukombozi, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Askofu Nyaisonga anabainisha kwamba, tangu awali, vijana wamekuwa na mchango wa pekee kabisa katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Siku ya Vijana Kijimbo kwa mwaka huu imekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, changamoto kwa vijana kuifahamu, kuiadhimisha, kuimwilisha katika matendo adili na kuisali. Nchini Tanzania, mchakato wa kuandika Katiba Mpya inayotarajiwa kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 unaendelea. Hii ni sheria mama.

Askofu Nyaisonga amewakumbusha vijana kwamba, Katiba nzuri ni ile iliyoandikwa na kuridhiwa na wananchi wenyewe, ili iweze kuwa ni dira na mwongozo katika maisha yao, daima wakiwa tayari kuilinda na kuitetea kwa udi na uvumba. Baada ya kuchangia maoni yao, sasa wanahamasishwa kujitokeza kujiunga katika Mabaraza ya Katiba, ili kuchangia katika maboresho ya Katiba itakayokuwa ni mhimili mkuu wa sheria za nchi.

Utakapofika wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu muswada wa Katiba Mpya, wananchi na hasa vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi. Hii inatokana na ukweli kwamba, vijana wengi hawapendi kujishughulisha na masuala yanayowahusu wakidhani kwamba, hayo ni mambo ya wazee, lakini huu ni wajibu wao wa kiraia na kijamii wanaopaswa kuutekeleza kwa umakini mkubwa.

Askofu Nyaisonga amewataka vijana ambao kwa sasa wanaunda kundi kubwa la wasomi wa Tanzania kujitokeza kuchangia katika mijadala ya Muswada wa Katiba, wakiongozwa na vipaumbele vya kitaifa yaani: mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu; umoja, upendo, udugu na mshikamano wa kitaifa. Wasimame kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini na kamwe wasikumbatie udini unaoweza kujitokeza katika Muswada wa Katiba, hata ikiwa ni kwa ajili ya dini yao, kwani hapa kuna hatari kubwa ya kuligawa taifa kwa misingi ya udini, ukabila na mahali anapotoka mtu.

Ikiwa kama mambo haya msingi hayataonekana katika Muswada wa Katiba Mpya, vijana wanahaki yakupaaza sauti yao kuuliza, kulikoni? Na kwa hakika watasikilizwa kwani hii ni haki yao msingi, wakinyama ni kuridhia mambo ambayo yatakuwa ni hatari kwa siku za usoni.

Askofu Gervasi Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, ametumia fursa ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo kupembua wajibu wa vijana katika maisha ya kijamii. Anasema, kuna wakati nchini Tanzania kulivuma mauaji ya vikongwe kutokana na imani za kishirikina, watu wengi wakaa kimya wakidhani kwamba, jambo hili lilikuwa haliwagusi, lakini hofu na mashaka yakaendelea kujengeka miongoni mwa watanzania hasa miongoni mwa wazee.

Kukaibuka mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, baadhi ya watu wakadhani kwamba ni tatizo lililokuwa linawagusa watu wenye uchu wa mali na madaraka kwa kukumbatia imani za kishrikina, watanzania wengi wakaendelea kuyapuuzia matukio haya, kwa vile tu, hayakuwagusa moja kwa moja!

Katika miaka ya hivi karibuni, kukaibuka tena wimbi la mashambulizi na uharibifu wa Nyumba za Ibada na mali za Serikali na watu wa binafsi. Baadhi ya watu wakaanzisha mtindo wa kuchoma mali za watu! Watanzania wakaendelea kukaa kimya kana kwamba, hakuna jambo lililokuwa linatendeka! Kukaibuka malumbano na kashfa za kidini na hatimaye, dhuluma na mauaji ya viongozi wa kidini. Watanzania wakasema, haya ni matukio yanayotendwa na wahuni wachache! Lakini Askofu Nyaisonga anasema, kwamba, matukio yote haya yanafunja umoja, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, ambao Tanzania imekuwa ikijivunia kwa takrbani miaka 50 iliyopita.

Mambo hayakuishia hapa, kuna mwakilishi wa madaktari wakati wakidai haki zao, alikamatwa na kupigwa; hivi karibuni, mwandishi wa habari alikung’utwa kisawa sawa, hadi kupelekwa nje kwa matibabu ya dharura! Haya ni matukio yanayogusa taaluma na kimsingi wahusika wakuu ni vijana. Askofu Nyaisonga amewaonya vijana kutojiingiza katika masuala yanayopelekea uvunjifu wa misingi ya haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, bali wasimame kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Upendo na Mshikamano kati ya watu!

Askofu Nyaiosonga katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo yaliyohudhuriwa na umati mkubwa wa vijana kutoka Jimboni Dodoma, aligusia pia umuhimu na wajibu wa vijana katika maisha ya kiroho, kwa kuwataka kukuza moyo wa sala, ibada na tafakari ya Neno la Mungu. Amewakumbusha vijana kusali daima ili wasije wakatumbukia katika kishawishi, lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, vijana engi wanafurahia kutumbukia au kutumbukizwa katika majaribu, lakini daima wakumbuke kwamba, sala ni mkombozi wao!

Askofu Nyaisonga anaendelea kusema kwamba, vijana wengi wamekosa fadhila ya utii kwa wazazi, walezi na wakuu wao wakidhani kwamba, utii kwa sasa umepitwa na wakati, lakini utii ni fadhila muhimu sana katika maisha ya kijamii. Amekumbusha kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu. Kumezuka mtindo nchini Tanzania kwa baadhi ya watu kudai haki zao, kiasi hata cha kukiuka haki msingi za binadamu. Kuna baadhi ya vijana wanataka kujipatia sifa, lakini kwa bahati mbaya wanajikuta wakiwa wameponzwa, kwani sifa njema zinarandana na dira ya maisha ya mtu!

Askofu Nyaisonga amewataka vijana kamwe wasikate tama na maisha, matokeo yake ni kukengeuka na kupoteza dira na mwelekeo wa maisha, kiasi cha kujitumbukiza katika vitendo vya ovyo! Vijana waongozwe na dhamiri nyofu, wawe na msimamo wa maisha na kamwe wasifuate upepo wa makundi ya vijana wenzao. Kila jambo walipime kwa umakini na busara kubwa na kamwe wasitafute njia ya mkato katika maisha, hii itawaponza! Kuna vijana wenye tamaa ya kupata maendeleo kwa haraka, lakini matokeo yake wanajikuta wakizama katika mambo ya ovyoooo!

Huu ni wakati wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Askofu Nyaisonga anasema, kuna baadhi ya vijana wamejikuta wakiwa ni watumwa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia: ni watumwa wa Computer na simu za viganjani, ni watu waliobobea katika mawasiliano yasiyo na tija! Baadhi yao wanajiamini mno kupita kiasi; hawashauriki wala kuonyeka!

Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma ameyatumia Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kutoa Katekesi ya kina na dira makini kwa vijana, akitambua kwamba, wao ndio jeuri na nguvu ya mabadiliko hasi na chanya ndani ya Jamii. Wanawajibika kushiriki kikamilifu katika majukumu yao kijamii na kiroho!








All the contents on this site are copyrighted ©.