Vijana salini kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume
wake!
Katika Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Siku ya Vijana Kijimbo na mwanzo wa Juma
kuu, linalowapatia Wakristo fursa ya kutafakari Mafumbo Makuu ya Ukombozi, Kardinali
John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Jumapili iliyopita tarehe 24 Machi
2013, aliwataka vijana kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye
ameonesha mapendo makuu kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika utume
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko tangu akiwa
nchini Argentina alikuwa na mapendo makuu kwa vijana na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii, ni kiongozi ambaye ana mguso wa pekee kwa vijana. Katika Maadhimisho ya
Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kardinali Njue aliwakumbusha vijana kwamba, tema iliyokuwa
inaongoza Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 ni changamoto inayowataka vijana kujitosa
kimaso maso kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yao.
Itakumbukwa kwamba, mji wa Rio de Janeiro, Brazil, utaanza kutimua
vumbi kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani hapo tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai
2013. Katika mahubiri yake Kardinali Njue amewataka vijana kujifunza kwa namna ya
pekee, Maandiko Matakatifu, kuyatafakari na hatimaye kuyamwilisha katika uhalisia
wa maisha yao kama wafuasi amini wa Kristo.
Haya ndiyo matumaini ya wazazi,
walezi na viongozi wao wa Kanisa. Vijana imara na thabiti katika imani, matumaini
na mapendo ni dalili njema ya kuwa na Mapadre na Watawa wanaoweza kujitoa bila ya
kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao.
Kardinali John Njue ambaye wakati
wa uchaguzi mkuu nchini Kenya alikuwa anashiriki kwenye Conclave mjini Vatican na
hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akachaguliwa, amewapongeza vijana nchini Kenya
kwa kulinda na kudumisha amani na utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi nchini
Kenya.