2013-03-27 08:36:50

Ushuhuda wa upendo kwa wote wanaotazamwa na Jamii kwa jicho la kengeza!


Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Alhamisi kuu jioni, Siku ambayo Yesu mwenyewe aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu; Sakramenti zinazofumbatwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na watoto walioko kwenye Gereza la Casal del Marmo. Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada hii pamoja na Kardinali Agostino Vallini, Makamu wa Askofu, Jimbo kuu la Roma.

Alhamisi kuu ni siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka ile zawadi ya upendo ambayo Kristo mwenyewe aliwaachia wafuasi wake, akiwataka kuhudumiana kwa upendo, kama kielelezo makini cha ufuasi wao kwake. Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha Ibada hii ya Misa Takatifu ya Alhamisi, Jioni ile siku iliyotangulia kuteswa kwake Yesu Kristo sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, changamoto ya kuonesha imani tendaji katika matendo ya huruma. Ni utume wa kuendeleza kutoa huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ibada hii inatarajiwa kuanza hapo saa 11:30 kwa Saa za Ulaya na kuhudhuriwa na vijana wapatao 50. Baba Mtakatifu Francisko ataosha miguu ya vijana kumi na wawili walioteuliwa kutoka hapo Gerezani kama kielelezo cha huduma endelevu hasa kwa maskini na wote wanaosumizwa pembezoni mwa Jamii; watu ambao wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kadiri ya Mafundisho ya Yesu mwenyewe. Hapa vijana watakuwa na uwakilishi wa kimataifa. Wao wenyewe ndio watakaosoma masomo na kusali sala ya waamini.

Baada ya Ibada ya Misa takatifu, Papa Francisko ataungana na Jumuiya ya Gereza hili na kusalimiana nao. Kutakuwepo pia na viongozi kadhaa kutoka Serikali ya Italia. Vijana hawa tayari wamekwisha andaa zawadi ya Msalaba wa mbao na kiti cha kupigia magoti, ambacho wamekitengeneza kwa mikono yao wenyewe hapo gerezani.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwpatia vijana hawa zawadi ya Pasaka kwa Mwaka 2013, lakini wao wanasema, zawadi kubwa kuliko zote maishani mwao ni uwepo wake wa kibaba! Haya ndiyo matumaini ya Mama Paola Severino, Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, wakati akihojiwa na Radio Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, tangu alipochaguliwa ameonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, wale ambao kimsingi Jamii inawataza kwa jicho la makengeza. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya vijana hawa ni kuwajengea tena matumaini mapya katika maisha yao.

Kati ya watoto waliofungwa gerezani humo ni wale wanaotoka nchi za nje, kiasi kwamba, wanasikia upweke na kukosa faraja kutoka kwa wazazi, ndugu na jamaa zao. Baba Mtakatifu Francisko atakuwa kweli ni faraja kubwa kwa watoto hawa katika hija ya maisha yao. Hawa ni vijana ambao wamepoteza dira katika maisha na kujikuta wako gerezani, wanapaswa kusaidiwa ili waweze tena kujenga uhusiano mwema na hatimaye, kurudi tena katika Jamii, wakiwa wamebadilika na kuwa watu wema zaidi.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kunako tarehe 18 Machi 2007 alitembelea Gereza la Watoto la "Casal del Marmo" na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na watoto waliofungwa gerezani hapo kwenye Kikanisa cha Baba Mwenyehuruma, changamoto inayoendelea kufanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko anayewahimiza waamini kuonesha huruma na kuguswa na matatizo ya jirani zao, kama sehemu ya mchakato wa kuijenga dunia ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.








All the contents on this site are copyrighted ©.