2013-03-27 07:56:27

Majadiliano kati ya waandishi wa habari na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI wakati wa hija zake za kichungaji


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa hija zake za kichungaji sehemu mbali mbali za dunia, alikuwa anapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Mazungumzo na waandishi wa habari yanaanzia katika hija yake ya kichungaji iliyofanyika mwezi Agosti 2005, alipokwenda Ujerumani ili kuhudhuria na kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amefanya hija ya kichungaji mara ya mwisho alipotembelea nchini Lebanon, ili kuzindua rasmi matunda ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya Kati, iliyokuwa imefanyika hapa mjini Vatican.

Kimsingi, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, amebahatika kufanya hija za kichungaji mara 24. Akatembelea: Uturuki, Brasil, Marekani, Australia, Cameroon, Angola, Yordani, Benin, Mexico na Cuba. Barani Ulaya, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alitembelea Poland, Hispania, Austria, Ufaransa, Jamhuri ya Wananchi wa Cheki, Malta, Ureno, Cyprus, Uingereza, Croasia na Ujerumani.

Mazunguko yote yaliyofanyika kati ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita na waandishi wa habari, kwa sasa yamekusanywa katika kitabu kilichoandikwa na Angela Ambrogetti na kuchapishwa na Idara ya Uchapaji ya Vatican, “Libreria Editrice Vaticana.” Lengo anasema mwandishi wa kitabu hiki, ni kutaka kufanya upembuzi wa dhati wa mawazo ambayo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ametoa kwa vyombo vya habari kimataifa katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hii ni nafasi nyingine tena ya kuendelea kujitaabisha kumfahamu kwa undani zaidi Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Ule utashi wake wa kutaka kuzungumza na vyombo vya habari ni habari tosha kabisa! Kama wanavyosema waswahili kwamba, “hii ndiyo habari”. Ni kitabu ambacho kimepambwa kwa picha mbali mbali za Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akiwa na wenzi wake wake wa safari ambazo kwa kawaida zilikuwa ni ndefu na za kuchosha!

Itakumbukwa kwamba, Angela Ambrogetti alikwisha andika kitabu kingine ambacho ni mkusanyiko wa mahojiano maalum kati ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili pamoja na waandishi wa habari. Kitabu hiki kwa sasa kimekwisha tafsiriwa katika lugha mbali mbali!

Idara ya uchapaji ya Vatican, hivi karibuni, imechapisha pia mkusanyiko wa katekesi za Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alizozitoa kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kuanzia Mwezi Oktoba 2012 hadi Mwezi Februari 2013. Lengo la Mwaka wa Imani, ni kuwasaidia waamini kufufua tena ndani mwao ile ari na mwamko wa imani yao kwa Yesu Kristo, Mkombozi pekee wa ulimwengu! Ni changamoto kwa waamini kutembea katika njia ile ambayo Yesu mwenyewe amewaonesha, daima wakijitahidi kutolea ushuhuda ile imani tendaji na nguvu za imani zinazioleta mabadiliko kati ya watu!

Kitabu hiki kina mkusanyiko wa katekesi 19 zilizotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kati ya tarehe 10 Oktoba 2012 wakati wa uzinduzi wa Mwaka wa Imani, hadi tarehe 27 Februari 2013, alipowaaga waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Hapo, akafunga ukurasa wake wa kuonekana hadharani na waamini, akapanda kwenda mlimani ili kusali na kutafakari kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo!








All the contents on this site are copyrighted ©.