Jitahidini kuwa Wakristo na Wakatoliki kweli kweli kwa maneno na matendo yenu!
Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi wa Jimbo kuu la Roma, anasema, alipoteuliwa na Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma, mawazo
yake yaliruka moja kwa moja hadi kwa Mtakatifu Monica, ambaye katika maisha alitamani
kumwona Mwanaye mpendwa Augustino aliyekuwa ametopea katika malimwengu akiwa Mkristo
na Mkatoliki kweli kweli; katika maneno na matendo yake. Hakuwa na jambo jingine
ambalo alilitamani katika ulimwengu huu ambao kwake ulisheheni magumu na majonzi tupu!
Mama Monica alifurahi sana aliposikia kwamba, Mwanaye Augostino ameongoka na baadaye
ameteuliwa kuwa Askofu. Hii ni furaha kubwa iliyokuwa inavuka matumaini na matarajio
yake. Askofu msaidizi Leuzzi anasema hiki ni kielelezo makini cha matamanio ya
Mama mwenye imani na matumaini thabiti, tunu ambazo kwake amezipokea na kama kielelezo
kikubwa cha zawadi ya imani katika hija ya maisha yake. Pengine kwa walimwengu jambo
hili linaweza kuonekana kuwa ni la kawaida sana, lakini mwamini kutambua kwamba, ameitwa
kuwa Mkristo Mkatoliki, ni jambo ambalo linapita ufahamu na matamanio yake ya kibinadamu.
Kuwa Mkatoliki wa kweli haimaanishi kufuata sheria na kanuni zinatolewa na Mama
Kanisa, bali ni kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ameandaa njia makini inayopania kujenga
na kuimarisha uhusiano na upendo wa dhati; kwa kujitoa bila ya kujibakiza. Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema, uhusiano huu unajikita katika Fumbo la
Msalaba, linaloonesha upendo wa Mungu kwa binadamu; upendo unaomkirimia mwanadamu
utimilifu wa maisha yake na kumwokoa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Askofu
msaidìizi Leuzzi anayasema haya katika barua yake ya kichungaji kwa wanafunzi wa Vyuo
Vikuu vilivyoko Roma. Anakumbusha kwamba, mwanadamu anaweza kuanza kumtafuta Mwenyezi
Mungu kwa njia ya kazi ya uumbaji ambayo kimsingi inachapa ya Mungu mwenyewe; kwa
kujiuliza maana ya maisha na Fumbo la Kifo. Lakini ikumbukwe kwamba, kwa njia
ya Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu amejitaabisha kumtafuta mwanadamu katika mapito yake
kabla ya mwanadamu mwenyewe kuanza kumtafuta Mwenyezi Mungu. Furaha ya kweli ni pale
mwamini anapomtambua Kristo kuwa ni Bwana na Mwalimu, kama alivyofanya Mtakatifu Magdalena,
alipokutana na Yesu Mfufuka! Kuna ”vigogo” waliotema cheche na sera zilizokuwa
zinapania kwa namna ya pekee kumpatia uhuru mwanadamu kutokana na vifungo vya kidini;
kama ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unavyotaka kuwasadikisha
watu wa nyakati hizi, bila kusahau pia kwamba, hata elimu inaweza kumtumbukiza mwamini
katika ombwe hili. Mwenyezi Mungu daima amemwacha mwanadamu katika uhuru wake na wala
hakutaka kumfunga na sheria na utashi wa kumpenda na kujitoa kwake bila ya kujibakiza.
Mwenyezi Mungu amependa kumwonjesha mwanadamu upendo wake, kama sehemu ya mchakato
unaopania kujenga na kuimarisha uhusiano wa dhati kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu.
Huu ndio uhuru unaoonesha katika kupenda na wala si kuwa mtumwa katika kupenda! Upendo
wa Kristo unamwongoza mwamini katika uhuru kamili dhidi ya upendo ambao wakati mwingine
ni kama ndoana; nipe nikupe! Anampenda mwanadamu kutoka katika undani wake, ili
kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano. Kristo anapenda kwa sababu anasukumwa na
upendo unaomkirimia mwamini uhuru kamili, ili aweze kujitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya huduma kwa Mungu na jirani kama alivyofanya Mtakatifu Augustino, Askofu na
Mwalimu wa Kanisa. Waamini wanaanza hija ya ukombozi kwa kupakwa majivu na itakamilika
katika Kesha la Pasaka, pale Mwenyezi Mungu atakapomshangaza mwanadamu kwa kumfufua
Yesu kutoka katika wafu. Kila mtu anapaswa kutambua kwamba, ana thamani kubwa machoni
pa Mungu, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wake. Kila mtu yuko huru, kupenda na kuhudumia
pamoja na kuwa mdau katika mapambano ya maisha yake kiroho na kimwili katika historia.
Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wanakumbushwa kuwa, katika
hija ya maisha yao kuna Kiongozi na Mwalimu anayewaonesha dira na njia ya kupitia,
changamoto kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Augustino, kusimama kidogo, kutafakari na
kumpokea Kristo, bila shaka kila mmoja wao, atafurahia kuwa Mkristo Mkatoliki, si
tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake!