2013-03-26 07:48:32

Serikali ya Brazil yamkaribisha Papa Francisko kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, 2013


Rais Dilma Rousseff wa Brazil ni kati ya viongozi wakuu wan chi waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu, wakati Papa Francisiko alipokuwa anaanza utume wake kama Askofu wa Jimbo la Roma hapa mjini Vatican hivi karibuni. RealAudioMP3
Katika mazungumzo ya faragha, Rais Rousseff alimwalika kwa mara nyingine tena Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Brazil wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 itakayofanyika mjini Rio de Janeiro kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013.
Inakadiriwa kwamba, zaidi ya Vijana million 4 kutoka sehemu mbali mbali za dunia watashiriki katika tukio hili la Imani kati ya Vijana na Kanisa. Katika mkutano wa viongozi hawa wawili, Baba Mtakatifu alimpatia zawadi Rais wa Brazil, Kitabu chenye mkusanyiko wa hati za Mkutano mkuu wa Aparecida, kama matunda ya mkutano mkuu wa tano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean uliofanyika mjini Aparecida, Brazil, mwezi Mei 2007.
Nakala ya Kitabu hiki alipewa pia alipewa Rais Cristina Fernàndes de Kirchner wa Argentina. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Jorge Mario Bergoglio alichangia sana katika kukusanya maoni na hatimaye, kuchapisha kitabu hiki ambacho kwa sasa ni rejea katika maisha na utume wa Kanisa.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipofanya hija yake ya kwanza Amerika ya Kusini, alitumia fursa hii pia kufungua mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean uliojikita zaidi katika changamoto za Uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo. Kitabu hiki kimesheheni tafakari za kichungaji zilizofanyiwa upembuzi yakinifu katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini mintarafu hali ya Kijamii kwa sasa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linasema Shirika la Habari za Kanisa Zenit kwamba, linaendelea kushirikiana na Vatican katika kupanga ratiba rasmi la Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Kwa wakati muafaka, Baba Mtakatifu Francisko atatoa ratiba ya hija yake ya kichungaji nchini Brazil kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.








All the contents on this site are copyrighted ©.