Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana ili kudhibiti biashara ya silaha kimataifa
Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa,
akishiriki katika mkutano kuhusu mkataba wa biashara ya silaha kimataifa, anawaalika
wajumbe kushirikiana kwa pamoja ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kuandika
ukurasa mpya wa historia kwa kupitisha mkataba huu. Lengo ni kujenga mazingira yatakayosaidia
kudumisha amani na utulivu; mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza.
Tangu
awali, ujumbe wa Vatican kwenye mikutano kama hii, umekuwa ukikazia umuhimu wa Jumuiya
ya Kimataifa kudhibiti biashara ya silaha kimataifa kupelekwa kwenye maeneo ambayo
yana migogoro, kinzani na vita, kwani uwepo wa silaha hizi umekuwa ni chanzo kikubwa
cha uvunjaji wa haki msingi za binadamu. Mafao ya kiuchumi yamekuwa yakipewa kipaumbele
cha kwanza dhidi ya maisha ya binadamu na familia yake.
Ni wajibu kwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati makubaliano
haya ya Umoja wa Mataifa katika udhibiti wa biashara ya silaha kimataifa. Badala ya
kuwa na kikundi cha watu wachache wanaodhulumiwa, ujumbe wa Vatican unapenda kupanua
wigo ili watu wengi zaidi waweze kufaidika na ulinzi unaobainishwa kwenye Mkataba
huu.
Kundi hili linawagusa: wanawake na wanaume; watoto, wazee na walemavu;
wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum; makabila na dini zenye waamini wachache.
Wote hawa wanapaswa kulindwa dhidi ya biashara haramu ya silaha inayopelekea uvunjwaji
wa haki msingi za binadamu na sheria. Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu silaha unatarajiwa
kufungwa rasmi hapo tarehe 28 Machi 2013, huko New York, Marekani, kwenye Makao Makuu
ya Umoja wa Mataifa.