Wanawake ni vyombo vya upatanisho, haki na amani katika Jamii
Mama Tunu Mizengo Pinda, Mke wa Waziri mkuu wa Tanzania, hivi karibuni alibahatika
kutembelea Radio Vatican na kujionea shughuli zinazoendeshwa na Radio hii katika
medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.
Hili ni jukwaa
la majadiliano ya kidini na kiekumene kati ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali.
Ni sauti ya wanyonge, inayopania kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, upendo,
amani na mshikamano wa dhati, ili dunia iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Katika
mahojiano na Radio Vatican, Mama Tunu Pinda anawaalika wanawake kwa namna ya pekee,
kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano, kwa kuanzia katika
familia zao. Hii inatoka na ukweli kwamba, Mama ni mdau wa kwanza katika kulinda na
kudumisha misingi bora ya maisha tunu za kifamilia.
Anasema, Familia zinaweza
kutekeleza dhamana na wajibu wake, ikiwa kama zitakuwa zimesimikwa katika uchaji wa
Mungu, maadili na utu wema. Malezi makini ya watoto hayana budi kuanzia katika Familia,
kwani Familia imara na thabiti ni nguzo ya Jamii imara na chemchemi ya viongozi bora
na shupavu wanaoweza kujitoa kikamilifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wao.
Mama Tunu Mizengo Pinda anawaalika wanawake kwa namna ya pekee, kusimama
kidete kulinda na kutetea haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati ndani ya Familia,
wao wenyewe wakiwa mstari mbele.