Vijana, tukutane, Rio de Janeiro, Julai, hapo patakuwa ni patashika nguo kuchanika!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, tarehe 24
Machi 2013, aliungana na waamini, mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kusali kwa pamoja Sala ya Malaika wa Bwana. Kwa
namna ya pekee, aliwaomba waamini kumwomba Bikira Maria aweze kuwasindikiza katika
hija ya Maadhimisho ya Juma kuu, ambamo Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo ya Ukombozi.
Bikira
Maria ni Mama aliyethubutu kuambatana na Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo katika Njia ya
Msalaba, hadi pale Mlimani Kalvari; huku akimsindikiza Mwanaye kuubeba Msalaba wake
kwa imani, utulivu na upendo mkuu, hadi katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka.
Baba
Mtakatifu anamwomba Bikira Maria Mteswa, aweze kuwasindikiza pia wale wote wanaokabiliana
na hali ngumu ya maisha. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbuka
na kuwaombea wagonjwa wa Kifua Kikuu; huku akiungana na Jumuiya ya Kimataifa iliyokuwa
inaadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "Zuia
nisipate Kifua Kikuu". Shirika la Afya Duniani, linabainisha kwamba, ugonjwa wa Kifua
Kikuu unaendelea kusababisha vifo na madhara makubwa katika Jamii.
Baba Mtakatifu
amewaweka vijana ambao walikuwa wanaadhimisha Siku ya Vijana Kijimbo, chini ya ulinzi
na maombezi ya Bikira Maria, akawataka kujiandaa kikamilifu katika maisha yao ya kiroho
katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani, itakayofanyika mjini Rio de Janeiro
kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013. Anawatakia vijana hija yenye furaha.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mtandao wa twitter, anawaalika vijana
kutoka sehemu mbali mbali za dunia kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku
ya Vijana Duniani, itakayofanyika nchini Brazil. Anawaasa vijana kuwa macho na kamwe
wasikubali kishawishi cha mwovu shetani kwamba, hawawezi kufanya chochote dhidi ya
vitendo vya jinai, ukosefu wa haki msingi za binadamu na dhambi!