2013-03-25 11:58:50

Kardinali Pengo aadhimisha Ibada ya Jumapili ya Matawi Jimboni Zanzibar na kutoa salam za Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisiko hivi karibuni, alikutana na kuzungumza na wawakilishi wa dini na madhehebu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, akikazia kwa namna ya pekee majadiliano katika upendo na ukweli na kwamba, Kanisa Katoliki linapania kujenga na kuimarisha majadiliano ya kidini na kiekumene na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Kanisa linapenda kujielekeza pia katika majadiliano na wale wasiokuwa na dini maalum, ambao daima wana kiu ya kutaka kumfahamu Mungu kutoka katika undani wao.

Baba Mtakatifu Francisiko anakumbusha kwamba, Wakristo na Waislam wana mwamini Mungu mmoja, aliye hai ambaye pia ni mwingi wa huruma na upendo; waamini wa dini hizi wanamwendea wote kwa njia ya sala, changamoto ya kujenga na kudumisha ushirikiano wa dhati baina ya Wakristo na Waislam kwa ajili ya mafao na ustawi wa binadamu wote. Kuna haja ya kuendeleza urafiki na heshima kila mtu; daima wakisimama pamoja kulinda na kutetea kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amedhaminishwa na Mwenyezi Mungu.

Wakristo na Waislam anasema Baba Mtakatifu Francisko, wanaweza kujibidisha zaidi kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujikita katika upatanisho na ujenzi wa amani ya kudumu; lakini jambo la msingi ni kushirikiana kwa pamoja ili kuzima kiu ya uwepo wa Mungu inayooneshwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Hii ndiyo changamoto ambayo Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam aliyopeleka Jimboni Zanzibar, katika Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, ambayo kwa mwaka huu, ilikuwa na nafasi ya pekee katika moyo wa Baba Mtakatifu Francisko aliyemtuma Kardinali Pengo kumwasilishia salam na matashi mema kwa Wakristo wa Zanzibar ambao wamepitia kipindi kigumu katika miaka ya hivi karibuni.

Kardinali Pengo katika mahubiri yake, kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu, Jimbo Katoliki la Zanzibar, amekazia kwa mara nyingine tena umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa dini mbali mbali nchini Tanzania na kamwe tofauti zao za kiimani zisiwe ni chanzo cha vurugu na chokochoko za kiimani. Hakuna mtu anayeweza kuhalalisha mauaji ya binadamu mwingine kwa madai ya kwamba, anatetea imani kwa Mungu aliye asili na uhai.

Kardinali Pengo ametumia fursa hii pia kuwataka Wazanzibar kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya sasa na yale ya kizazi kijacho. Kuna wakati Zanzibar ilikuwa inatoa maji safi ya kunywa, lakini sasa maji mengi ni ya chumvi. Utunzaji wa mazingira ni jambo linalopaswa kupewa msukumo wa pekee na Jamii na wala hawapaswi kulipuuzia.







All the contents on this site are copyrighted ©.