Jumapili ya Matawi: Kielelezo cha Furaha; Changamoto ya Kumfuasa Kristo Msulubiwa
na Vijana kujitosa kumtangaza Kristo hadi miisho ya dunia
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Matawi, aliongoza umati mkubwa wa waamini waliokuwa
wamefurika kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kushiriki katika Ibada ya Jumapili
ya Matawi, kielelezo cha kuanza Juma kuu. Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipoingia
mjini Yerusalemu, wafuasi wake walitandaza nguo zao njiani, wakaimba nyimbo za kumsifu
Mungu wakisema, Mbarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana, Hosana, Juu mbinguni. Amani
duniani kwa watu anaowaridhia.
Baba Mtakatifu anasema, umati mkubwa wa watu,
furaha na baraka ni mambo yanayoashiria furaha ya ndani inayobubujika kutoka kwa Yesu
Kristo, aliyeijaza mioyo ya watu matumaini. Hawa ni wale waliosahaulika, maskini na
"akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi! Yesu aliyafahamu mateso na mahangaiko
ya mwanadamu, akawaonesha uso wa huruma ya Mungu, aliyejinyenyekesha ili kuponya madhaifu
ya binadamu: kiroho na kimwili.
Huyu ndiye Yesu anayewaangalia wote: matatizo,
magonjwa na dhambi zao. Anaingia mjini Yerusalem akitaka kuwaonesha watu upendo wake
mkuu, unaowakumbatia watu wote katika furaha. Hii ndiyo furaha ambayo waamini kutoka
sehemu mbali mbali za dunia wameionesha wakati wa Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi,
kwa kumsindikiza Yesu, kwa kutambua kwamba, yuko kati yao, kama rafiki, ndugu na Mfalme
anayeangazia mapito ya watu wake.
Yesu ni Mungu aliyejinyenyekesha na watu
wanapaswa kumpokea kwa FURAHA, neno ambalo Baba Mtakatifu Francisiko amependa kulikazia
katika mahubiri yake, kwa kuwataka waamini kuwa ni watu wenye furaha na kamwe wasikubali
kukatishwa tamaa kwani hii ni furaha inayopata chimbuko lake kwa mwamini kukutana
na Yesu Kristo ambaye anaendelea kufanya hija na wafuasi wake, hata katika nyakazi
ngumu za maisha yao na pale wanapokutana na vizingiti.
Hapa ni mahali ambapo
waamini wanapaswa kuwa makini zaidi kwani Mwovu Shetani anaweza kuwajia akiwa amejivika
sura ya Malaika; kamwe waamini wasimsikilize wala kumfuata, bali waendelee kumsindikiza
na kufuasa Yesu Kristo chemchemi ya furaha ya kweli.
Baba Mtakatifu anawakumbusha
waamini kwamba, kamwe wasikubali kupokonywa tumaini linalobubujika kutoka kwa Yesu
mwenyewe. Yesu ni Mfalme, aliyeonesha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, changamoto
na mwaliko wa kumfuasa kwa imani na matumaini, huku wakiendelea kumtangaza kuwa ni
Mkombozi wa Ulimwengu. Anaingia mjini Yerusalem kwa shangwe, ili aweze kutimiza unabii
uliotolewa katika Maandiko Matakatifu, kwa kuteswa, kufa na hatimaye, kufufuka kutoka
katika wafu. Kristo alikufa Msalabani, mwaliko kwa waamini kukumbuka kwamba, wanamfuasa
Kristo Mfalme aliyetundikwa Msalabani.
Kwa kifo chakle Msalabani, Yesu amejitwika
dhambi na mapungufu ya mwanadamu, akayaosha kwa njia ya Damu yake Azizi, huku akiwaonjesha
waamini huruma na upendo wa Mungu. Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata
leo hii, bado kuna: vita, makosa ya jinai, kinzani za kiuchumi na kijamii inayoendelea
kuwaathiri zaidi wanyonge. Watu wanaonesha uchu wa mali na madaraka; wanaendelea kuogelea
katika rushwa na ufisadi; , migawanyiko pamoja na kuenzi utamaduni wa kifo na uharibifu
wa mazingira, bila kusahau dhambi za kila mwamini mmoja mmoja.
Watu wanakosa
upendo kwa Mungu, jirani na katika kazi ya Uumbaji. Msalabani, Yesu ameweza kukumbatia
yote haya kwa njia ya upendo wake mkuu unaoshinda dhambi na mauti na hatimaye kuonesha
ushindi kwa njia ya Ufufuko kutoka katika wafu! Huu ndio ushindi wa Kristo unaooneshwa
na Fumbo la Msalaba. Ni chemchemi ya furaha kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Msalaba,
watu wamekombolewa.
Baba Mtakatifu Francisiko aliwakumbusha waamini na mahujaji
waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
kwamba, Jumapili ya Matawi kwa Mwaka 2013, ilikuwa pia ni Siku ya Vijana Kijimbo,
kama sehemu ya Maandalizi ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani. Umati mkubwa wa vijana
umeshiriki katika maandamano ya Jumapili ya Matawi, ili kushiriki Siku kuu hii ya
Imani, kwa kuwashirikisha wengine ile furaha ya imani inayobubujika kutoka katika
moyo wa ujana.
Vijana wamemsindikiza Mfalme anayependa hadi upeo kwa njia ya
mateso na kifo cha Msalaba, changamoto kwa vijana kuhudumia na kupenda, bila kuuonea
aibu Msalaba wa Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujitosa kimasomaso kumshuhudia
Kristo ambaye ni chemchemi ya furaha yao ya kweli; Yeye ambaye ameshinda ubaya kwa
njia ya upendo. Vijana wanachangamotishwa kufanya hija ya Msalaba hadi miisho ya dunia;
huku wakiendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kwa njia ya Msalaba, Yesu amevunja
kuta za utengano kati ya watu; na badala yake amewakirimia upatanisho na amani.
Baba
Mtakatifu Francisiko amewahakikishia vijana kwamba, anaungana na watangulizi wake:
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika
hija ya Njia ya Msalaba. Anatarajia kukutana na umati wa vijana kutoka sehemu mbali
mbali za dunia, hapo Julai katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka
2013.
Huu utakuwa ni muda wa furaha na imani kwa vijana kuweza kuutangazia
ulimwengu jinsi inavyopendeza kumfuasa na kutembea na Yesu Kristo, kwa kujiondoa katika
ubinafsi wao, tayari kutangaza Injili ya Kristo. Baba Mtakatifu Francisiko amehitimisha
mahubiri yake kwa kukumbusha mambo makuu matatu: Furaha; Msalaba na Vijana.
Anawaalika
waamini kumwomba Bikira Maria aweze kuwafundisha kuwa ni watu wenye furaha kwa kukutana
na Yesu Kristo, ili kushiriki upendo wake ambao aliushuhudia alipokuwa pale chini
ya Msalaba. Waamini wajitahidi kuwa na moyo wa ujana katika maadhimisho ya Mafumbo
ya Kanisa katika Juma Takatifu.