Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, hivi karibuni amewaongoza Mapadre
katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta Matakatifu,: haya ni Mafuta
ya Wakatekumeni, Krisma ya Wokovu na Mafuta ya Wagonjwa. Ibada ambayo kimsingi inaadhimishwa
Alhamisi Kuu.
Hii pia ni fursa kwa Mapadre kurudia tena ahadi zao za utii kwa
Askofu Mahalia pamoja na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati wanaposhiriki
katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu waliokabidhiwa na Mama
Kanisa katika maeneo yao. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Katoliki Dodoma.
Katika Ibada hii, Askofu
Nyaisonga alibariki Mafuta ya Wagonjwa yatakayotumika kuanzia sasa kwa kuwataka waamini
kufahamu na kuthamini Sakramenti ya Mpako Mtakatifu. Kwa Waamini wagonjwa ambao wako
kufani, Sakramenti hii inapania kuwapatia neema ya pekee ili kuweza kukabiliana na
magumu haya yanayoweza kutokana na ugonjwa, uzee au hatari ya kifo. Matunda ya neema
ya Sakramenti hii ni kumwezesha mgonjwa kujiunga na mateso ya Kristo, kwa ajili ya
manufaa yake mwenyewe na kwa ajili ya mafao ya Kanisa.
Mwamini anajaliwa nguvu,
amani, ujasiri ili kuvumilia Kikristo mateso ya ugonjwa au uzee. Ni Sakramenti inayompatia
mwamini msamaha wa dhambi, ikiwa kama mgonjwa hakuweza kupata fursa ya kuungama dhambi
zake. Sakramenti ya Mpako Mtakatifu inamrudishia mwamini afya, kama inafaa kwa wokovu
wa kiroho. Ni Sakramenti inayomwandaa mwamini katika safari ya kuuendea uzima wa milele.
Askofu
Nyaisonga pia alibariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu yanayotumiwa wakati wa Sakramenti
ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Amewakumbusha Mapadre kwamba, wao ni wazee
na viongozi wa Kanisa; wanashiriki kwa namna ya pekee katika kulitumikia Kanisa kwa
kuadhimisha na kugawa Mafumbo ya Kanisa. Mapadre wakitenda kwa nafsi ya Kristo na
kulitangaza Fumbo lake, huyaunganisha maombi ya waamini na sadaka ya Kristo na kwamba,
huduma yao ya Kikuhani huchota nguvu kutoka katika Sadaka ya Kristo. Ni viongozi waliopewa
dhamana ya Kibaba ndani ya Kanisa.
Askofu Nyaisonga anasema kwamba, kwa vile
Mapadre ni waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa, wanapaswa kujitakatifuza
katika maisha yao, kwa kuambatana na Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu
na Maisha ya Kisakramenti. Mapadre wawe kweli ni kielelezo cha maisha adili na utakatifu
na kamwe wasiwe ni kikwazo kwa watu wanaowazunguka. Waamini nao wanapaswa kuwaheshimu,
kuwathamini, kuwaombea Mapadre wao na kamwe wasiwe ni kikwazo na chanzo cha kuanguka
kwao kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu.