Juma Kuu: Kumbu kumbu ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo
Kanisa linakianza kipindi cha Jumaa kuu, linalowapatia waamini fursa ya kuweza kutafakari
kwa kina kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Jumapili ya Matawi, Kanisa linakumbuka
siku ile Yesu, Masiha alipoingia mjini Yerusalem akiwa amepanda Punda, alama ya unyenyekevu
wa hali ya juu kabisa, huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao njiani. Ni
Siku ya Vijana Kijimbo! Ni matumaini ya Kanisa kwamba, vijana kutoka katika Parokia
mbali mbali pale inapowezekana, washerehekee siku hii wakiwa wamemzunguka Askofu wa
Jimbo lao. Hata katika ngazi ya Kiparokia, vijana wanaweza kuiadhimisha Siku hii kwa
kumzunguka Paroko wao! Kama mwaka huu hamkuweza kufaulu, basi jipangeni sawasawa hapo
mwakani! Waamini hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu, wanaendelea kuandamana
huku wakimshangilia Kristo Mfalme wa amani, huku wakiwa wamebeba matawi ya mitende
mikononi mwao; matawi yanayohifadhiwa kwa heshima, kama kumbu kumbu ya kuonesha uaminifu
wao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Hiki ni kipindi
cha tafakari ya kina, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa
Imani, changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anaifahamu imani yake, ili
aweze kuikiri, kuiadhimisha, kuimwilisha katika matendo adili na hatimaye, kuisali,
kama sehemu ya mchakato wa imani tendaji. Mara mbili kwa mwaka, Mama Kanisa anawapatia
Watoto wake fursa ya kuweza kusikiliza Mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristo yakisomwa
kwa Ibada kubwa: Ijumaa kuu na Jumapili ya Matawi. Liturujia ya Jumapili ya Matawi,
inaanza kwa kumshangilia Kristo, Hosana Mwana wa Daudi na baadaye, tunahitimisha kwa
kusema, mwondoe, mwondoe, Msulubishe! Hapa Yesu anatualika kushiriki katika ile
Saa yake ya mateso, ambayo kwa hiyari yake mwenyewe, anaamua kujitosa kimasomaso kuteswa
na kufa Msalabani na hatimaye, kufufuka siku ya tatu, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ndio mwanzo wa Injili unaojikita katika
mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Wasifu wa watu maarufu katika ulimwengu wetu unaanza
kwa siku yake ya kuzaliwa hadi pale anapoitupa mkono dunia! Lakini, kwa Yesu, wasifu
wake unaanza katika mateso, kifo na ufufuko wake. Hii ndiyo hazina ya Imani ambayo
vijana wanapaswa kurithishwa, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa.
Kifo cha Yesu kimetokana na dhambi za binadamu, ni wakati wa kukinywea kile Kikombe
cha mateso. Mateso ya Yesu yanawahusisha watu wengi: Yuda Iskarioti aliyemsaliti
kwa busu! Mtakatifu Petro aliyemkana mara tatu, Mitume waliotimua mbio walipoona amekamatwa
na kukokotwa kuelekea hukumuni, Pilato aliyenawa mikono akisema hausiki kabisaaa na
kifo cha Yesu, hata kama hakumkuta na hatia, lakini amestahili kufa! Huu ndio mwelekeo
wa wale wanaopindisha sheria kwa ajili ya mafao yao binafsi! Baraba anayeponea chupu
chupu kutoka katika tundu la sindano! Wevi wawili waliokuwa wametundikwa Msalabani.
Katika Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari, nje ya Mji, kulikuwepo na wanawake
wa Yerusalemu waliokuwa wanamlilia Yesu na pale chini ya Msalaba alikuwepo Bikira
Maria amesimama kwa ukimya. Kuna wengine waliokuwa mbali wanachungulia kuona kama
Yesu atawafanyia Suprise! Lakini, maskini, wakati huu, Yesu akaamua kubaki Msalabani,
ili kuchukua dhambi za binadamu. Kati ya wahusika mbali mbali tuliowasikia katika
Simulizi la Mateso ya Yesu, jiulize wewe uko sehemu gani? Tunaweza kufunga Injili
ya Mateso ya Yes una kurudi nyumbani kama walivyofanya wale watesaji na mashahidi
waliokwisha fariki dunia kitambo kirefu kilichopita. Pilato amekwisha ondoka mahakamani
pamoja na wazee wa Baraza. Lakini, mchakato wa hukumu ya Yesu bado unaendelea
miongoni mwa Wakristo wanaokumbana na madhulumu kutokana na imani yao kwa Kristo na
Kanisa lake; unaendelea kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; hukumu
hii inaendelea kwa wote wanaokumbatia utamaduni wa kifo na uharibifu wa mazingira.
Hukumu inaendelea kwa wote tunao endelea kutenda dhambi. Simulizi la Mateso ya
Yesu Kristo litukumbushe mambo makuu matatu: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo; changamoto
ya kuifahamu Kanuni ya Imani, ili tuweze kuiadhimisha kwa ushiriki mkamilifu, hali
tukijitahidi kuimwilisha katika matendo adili kwa kutambua kwamba, hii ni imani ambayo
tunaisali kama kielelezo cha ile imani tendaji ambayo ni dira na mwongozo wa maisha
yetu. Ninakualika kuchukua Msalaba wako kila siku ya maisha yako na kuanza kumfuasa
Yesu Kristo, changamoto ya kupyaisha imani yetu katika hija ya maisha yetu! Jamani,
kesheni pamoja na Kristo anapoanza Njia ya Msalaba! Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.