Askofu Mkude: Waamini shindeni Ubaya kwa njia ya kutenda wema, mkionesha imani thabiti
kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka!
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa makini kwa waamini kuifahamu, kuikumbatia,
kuishuhudia na kuwashirikisha wengine, ili waweze kumfahamu, kumpenda na kumtumikia
Kristo katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Ni changamoto
ya kukuza na kuendeleza zile ahadi za ubatizo ambazo waamini wanaapa wao wenyewe au
kwa niaba yao! Vinginevyo, imani kwa Kristo na Kanisa lake, inaweza kuzimika kama
kibatari na watu kuanza kuogelea katika giza la mauti na kifo!
Ni changamoto
iliyotolewa na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, wakati wa Ibada
ya Kubariki Krisima ya Wokovu, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Patris,
Jimboni Morogoro. Kimapokeo Ibada hii hufanyika Siku ya Alhamisi Asubuhi, Mapadre
pamoja na Waamini hushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki mafuta
matakatifu yaani "Krisma ya Wokovu" yatakayotumika kwa ajili ya Sakramenti ya Ubatizo,
Kipaimara, Daraja Takatifu na Mpako wa Wagonjwa.
Lakini kutokana na changamoto
za kichungaji, Majimbo mengi huiadhimisha Siku hii kabla, ili kutoa nafasi kwa Mapadre
kuadhimisha Alhamisi kuu kwa utulivu, wakikumbuka Siku ile Yesu alipoweka Sakramenti
ya Ekaristi Takatifu na Upadre, akawataka wazimwilishe Sakramenti hizi kwa njia ya
huduma kwa ndugu zao katika Kristo, lakini zaidi kwa wanyonge na wale wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Katika mahubiri yake kwa mujibu wa Radio Ukweli ya Jimbo
Katoliki Morogoro, Askofu Mkude amesema kwamba, watu wengi wanamezwa na malimwengu,
kiasi cha kukumbatia na kutoa kipaumbele cha pekee katika mali na madaraka, kiasi
cha kufisha maagano yao na Mwenyezi Mungu. Watu wa namna hii ni sawa na taa iliyozimika.
Kipindi
cha Kwaresima iwe ni fursa ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu; watu watumie nafasi
zinazotolewa na Mama Kanisa ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili dunia
iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani
uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, waamini
wajitahidi kutolea ushuhuda imani yao kwa njia ya matendo ya huruma hasa zaidi kwa
maskini wa kiroho na kimwili na wote wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu.
Kwa njia hii, waamini watakuwa wanajiwekea hazina mbinguni.
Kuhusu vurugu za
kidini nchini Tanzania, Askofu Mkude anawaalika waamini kushinda ubaya kwa wema. Kwa
njia hii waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kudumisha na kuimarisha
amani nchini Tanzania; amani ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imeanza kumeguka vipande
vipande kutoka na chokochoko za kidini.