Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni matokeo ya ushirikiano wa kimataifa
Jumuiya ya Kimataifa tarehe 22 Machi 2013 inaadhimisha Siku ya Maji Kimataifa. Wataalam
wa masuala ya maji na afya, chakula na lishe; umaskini na mazingira; ubaguzi na nyanyaso
dhidi ya wanawake; mwendelezo wa usawa na demokrasia ya kweli; kwa pamoja wanapenda
kuunganisha sauti zao kwa kusema maji ni uhai na mhimili mkuu katika medani mbali
mbali za maendeleo na maisha ya mwanadamu.
Kwa bahati mbaya maji sasa inaonekana
kuwa ni bidhaa adimu inayotafutwa kwa udi na uvumba katika soko la kitaifa na kimataifa,
lakini kwa bahati mbaya, kuna mamillioni ya watu ambao bado hayana uhakika wa maji
safi na salama. Jopo la watetezi wa haki msingi za binadamu linasema, kuna haja kwa
Jumuiya ya Kimataifa kutenga rasilimali itakayosaidia watu kutoka katika nchi zinazoendelea
duniani kuwa na uhakika wa maji safi na salama, kwa ajili ya maboresho ya huduma ya
afya; upatikanaji wa chakula pamoja na mapambano dhidi ya umaskini wa kipato na hali.
Kuna haja pia ya Jumuiya ya Kimataifa kuibua na kutekeleza mikakati ya utunzaji
bora wa mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho, ili kuendelea pia
kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya maboresho ya afya; jambo linalohitaji
ushirikiano wa dhati, sanjari na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Serikali hazina budi kutoa msukumo wa pekee kwa upatikanaji wa maji kutokana
na ukweli kwamba, waathirika wakuu wa ukosefu wa maji au umbali wa upatikanaji wa
maji ni wanawake. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na wala si tu bidhaa au
huduma!
Wataalam wa haki msingi za binadamu wanaialika Jumuiya ya Kimataifa
kuadhimisha Siku ya Maji Kimataifa, kwa kuweka mikakati ya matumizi bora ya maji yaliyopo
pamoja na kubainisha mbinu zitakazotumiwa ili watu wengi zaidi waweze kupata maji
safi na salama kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao