2013-03-22 07:34:19

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Matawi


Mpendwa mwana wa Mungu karibuni katika kipindi cha tafakari ya Neno la Mungu, tunapoadhimisha Dominika ya Matawi, Dominika ambayo ni mwanzo wa Juma Kuu, Juma la Pasaka.Kabla ya Misa Takatifu daima tunaanza kwa maandamano ambayo ni ishara ukumbusho wa kuingia kwa Yesu Kristu Yerusalemu. RealAudioMP3

Ni ishara ya utukufu kwa Mungu juu mbinguni. Mwaliko ambao Mama Kanisa anatupa ni ule wa kumshangilia Bwana na kuandamana tukimsindikiza kuelekea Yerusalemu. Kwa kawaida yaweza kuonekana tunafanya kumbukumbu tu lakini hivyo bali tunashika tunamsindikiza na kupata neema zote alizozitoa wakati ule na tunashika njia yetu ya kumfuasa yeye tukielekea Pasaka ya Mbinguni.

Kwa kawaida tunajua kuwa Kristu aliteswa akafa na kisha kufufuka, kumbe kwa njia hiyo tunapata tumaini na tunaalikwa kufuata nyayo zake daima mpaka kufa kwetu. Kwa jinsi hiyo njia ya Bwana ni njia yetu sote. MamaKanisa ametuwekea mateso makali ya Bwana mbele yetu ambayo yaweza kuwa ni tishio na hivi kujenga woga katika safari,hata hivyo hatuogopi maana ikiwa Bwana ambaye hakustahili alivumilia je sisi ambao twasitahili twaweza kukwepa wajibu huo? Si hilo tu bali pia matunda ya mateso makali ya Bwana tumeona ni wokovu wa ulimwengu.

Bwana anapokaribia kuingia Yerusalemu ili kumalizia njia yake ya mateso anapanda mwanapunda, hii ni ishara ya unyenyekevu, ishara ya kuwa yeye si mfalme wa mabavu bali anayetumia upendo kujibu ubaya wa ulimwengu. Hii haina maana kuwa hana uwezo bali uwezo wake ni kwa ajili ya wokovu wa watu na si wa mapigano ya kivita.

Watu wote wanatandaza nguo na majani ya mitende wanaimba Hosana mwana wa Daudi, hili ni shangilio kwa Mungu wa Mbinguni, ni kiitikio cha utukufu na ushindi wa Bwana. Kwa hakika ni mwendelezo wa shangilio ambalo malaika walilitoa kwa Mwana wa Mungu alipozaliwa pangoni Betlehemu. Lk 2:14 Jibu la shangilio hili ni amani yangu nawapa Yn: 14:27.

Nabii Isaya anapoagua juu ya Masiha anatuwekea Masiha aliye mvumilivu, anayetukanwa anayekupigwa na hata kung’olewa ndevu lakini hajibu mapigo, bali ametulia na kuweka tumaini kwa Mungu wake. Jambo hili linakamilika katika Bwana Yesu anapoingia Yerusalemu. Mwinjili Matayo anasema tazama maaskari wa Pilato wanavyomdhihaki Yesu Mkombozi” Mt. 27:27-31 Kwa jinsi hii Nabii Isaya anamtangaza Masiha mshindwa, mteswa, asiyeua lakini anayehuisha kwa upendo na kuleta wokovu.

Mtume Paulo anawaonya Wafilipi na kisha kuwaimarisha katika kuiga na kujifunza kwa Bwana. Katika familia ya Wafilipi kuna chuki, ugomvi na fitina na hivi anawapa wosia akisema kila mmoja amthamini mwenzake na kwa kukazia wosia huu anaweka mbele yao Yesu Kristu Masiha aliyejishusha mpaka kuwa mwanadamu na si ubinadamu tu bali hata kuteswa na Warumi! Chukua muda kidogo tafakari na fikiri juu ya upeo wa jambo hili!

Fikirini mtu bilionea akijishusha na kukaa na maskini! Kwa hakika mbele ya ulimwengu atakuwa wa ajabu lakini wa maana zaidi. Kristu kwa umwilisho wake hakupoteza Umungu wake bali ulibaki umejificha na hivi Mungu Baba akamwadhimisha mno kwa unyenyekevu wake. Basi mwaliko kwako ni amani na tulivu daima na Mungu atakuadhimisha mno!

Katika Injili ya Marko katika historia ya mateso anatuwekea Yesu Kristu asiyejibu ubaya wowote unaoelekezwa kwake au kwa wengine kwa nguvu za kivita bali kwa neno la upendo. Tazama dhihaka ya Yuda Iskariote, tazama mtume Petro anapotumia upanga kukata sikio la mtu aliye kinyume na Bwana. Yote haya anayajibu kwa utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu, rudisha panga alani!

Mwinjili Marko anatuonesha mitume wanaokimbia baada ya mambo kuwa magumu, wanamwacha Bwana, hii ni alama ya udhaifu, kutoelewa bado nini hasa mpango wa Mungu kwa ajili ya wokovu. Hawajaelewa bado kuwa lazima Bwana ateseke ndipo ukombozi wa ulimwengu utokee. Nasi ndugu zangu kuna wakati tunamatarajio makubwa ya ustawi na hivi kunapotokea ugumu katika imani tunakimbia au tunaanza malalamiko na hata kuleta vulugu katika jumuiya.

Basi mpendwa mwana wa Mungu, kukimbia kwa Mitume ni kumwacha Bwana katika upweke, vivyohivyo kukimbia kwetu ni kumwacha Bwana akisononeka na kuumia moyoni na hasa kundi lake katika upweke wa kukosa mapendo ya kichungaji.

Mwinjili Marko anatupa jambo jingine jema kwa ajili ya Imani, pale ambapo Bwana anapokata roho na akida mpagani anatangaza hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu Mk. 15:39 Manaeno haya yanatamkwa na mpagani na wakristu wa karne za kwanza watayatumia katika kutangaza imani yao katika Yesu Kristu. Mpagani huyu anawawakilisha wale wote wanaotafuta imani katika Bwana, yaani wongofu wao hauji kwa sababu ya miujiza bali wanaelewa nini maana ya upendo na nini maana ya mtu kujitoa maisha kwa ajili ya wengine.

Alama ya kupasuka kwa pazia la hekalu vipande viwili toka juu hadi chini Wainjili watuambia kuwa kwa njia ya kifo cha Bwana mipaka kati yetu na Mungu imeondolewa na si tu kati ya Mungu nasi bali kati yetu sisi kwa sisi. Tangu siku anakufa msalabani wote tu wana wa familia moja ya Mungu.

Mpendwa mwanatafakari ukiyakumbuka mateso ya Bwana na kuyaweka moyoni na kisha kuyaunganisha mateso yako na yake basi pasaka kwako ni ufufuko kweli. Ninakualika basi umsindikize Bwana katika wiki hii kuu kwa furaha na utulivu mkamilifu ili mwisho wa mateso tupate matunda ndiyo uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.