2013-03-22 12:02:20

Siku ya Misitu duniani na changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa siku za usoni!


Kwa mara ya kwanza Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 21 Machi 2013 imeadhimisha Siku ya Misitu Duniani na changamoto kutoka kwa Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kuhakikisha kwamba, sheria inachukua mkondo wake ili kukomesha uharibifu wa misitu sehemu mbali mbali za dunia.

FAO inasema kwamba, misitu iliyoko katika Ukanda wa Mediterannia iko hatarini kutoweka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Utunzaji bora wa misitu na mazingira kwa ujumla unaweza kusaidia katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na magonjwa kwa kuwa na maendeleo endelevu. Udhibiti wa uharibifu wa misitu ni ajenda inatakayofanyiwa kazi kwa kasi kubwa baada ya kukamilisha Malengo ya Maendeleo ya Millenia, hapo mwaka 2015.

Athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la idadi ya watu ni mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kutoweka kwa misitu ya asili, hali ambayo inaweza kuhatarisha ustawi na maendeleo ya watu sehemu mbali mbali za dunia.Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati wa kutunza misitu, ili iweze kuendelea kutoa huduma makini kwa Familia ya binadamu. Lengo hili linaweza kufikiwa kwa kudhibiti uchomaji wa misitu, hali ambayo inapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira.







All the contents on this site are copyrighted ©.