2013-03-22 08:33:54

Papa akutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda mjini Vatican


Waziri mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania amekutana na Papa Francisko na kufanya naye mazungumzo ya faragha ikiwa ni pamoja na kuwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Mkuu alipata fursa hiyo Alhamisi, Machi 21, 2013 alipofika kwenye makazi ya muda ya Papa Francisko yaliyoko Domus Sanctae Marthae mara baada ya kumaliza vikao na wawakilishi kadhaa wa mashirika ya kimataifa walioko mjini Roma, Italia.

Katika mazungumzo yao, Waziri Mkuu alimweleza Papa Francis kwamba amefika kuwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Kikwete. Katika salamu hizo, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Rais wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete anakutakia heri katika jukumu hili jipya ulilopewa na Mwenyezi Mungu. Tunamshukuru Mungu kwa kukupa jukumu la kulea Kondoo wa Kristo, nasi tutaendelea kukuombea katika utume huu mkubwa ulionao.”

Waziri Mkuu alimweleza Papa Francisko kwamba, Rais Kikwete alitamani kuwepo kwenye ibada yake ya kusimikwa rasmi lakini kutokana na majukumu mengine ya kitaifa aliyokuwa nayo, hakuweza kufika na badala yake amemuomba Waziri Mkuu amuwakilishe.

Akipokea salamu hizo, Papa Francisko alisema anatambua fika jinsi Tanzania inavyojitahidi kuendeleza amani chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. “Tutaendeleza ushirikiano wa karibu uliokuwepo baina ya nchi zetu,” alimalizia Papa Francisko.

Waziri Mkuu Pinda na ujumbe wake, walipata pia nafasi ya kuonana na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Pinda wakati wa ziara yake mjini Roma alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza pia na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Bwana Josè Graziano da Silva, kwenye Makao Mkuu ya FAO, hapa mjini Roma. Alitembelea pia Ofisi za Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP siku ya Jumatano, tarehe 20 Machi 2013.









All the contents on this site are copyrighted ©.