Wananchi wa Zimbabwe wanaunga mkono Katiba Mpya kwa 95%
Asilimia 95% ya wananchi wa Zimbabwe wanaunga mkono muswada wa Katiba Mpya ya Zimbabwe.
Haya ni matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa nchini Zimbabwe mwishoni mwa juma. Lengo
ni kupunguza madaraka makubwa ya Rais, ambaye ataweza kuwaongoza wananchi wa Zimbabwe
kwa vipindi viwili tu!
Kwa upande wake, Rais Robert Mugabe, mwenye umri wa
miaka 89 bado anaruhusiwa kikatiba kuwaongoza wananchi wa Zimbabwe, kwani sheria hairudi
nyuma, ingawa Rais Mugabe amekuwepo madarakani tangu mwaka 1980, Zimbabwe ilipojinyakulia
uhuru wake kutoka kwa Waingereza.
Upatikanaji wa katiba mpya ni hatua kubwa
ya maendeleo ya kidemokrasia na utawala bora ambao umewagharimu sana wananchi wa Zimbabwe
katika kipindi cha miaka michache iliyopita! Zimbabwe iliyokuwa inajivunia maendeleo
na ustawi wa wananchi wake, ikajikuta inachechemea katika kinzani na misigano ya kisiasa
na kijamii; matukio yaliyokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu nchini Zimbabwe.
Katiba
Mpya ya Zimbabwe inatoa madaraka makubwa kwa Bunge la Zimbabwe ambalo kwa sasa lina
idadi kubwa ya Wabunge kutoka katika Chama cha Upinzani. Kimsingi, Katiba inatoa kipaumbele
cha kwanza kwa heshima na utu wa binadamu, haki msingi, uhuru wa mtu, dhamiri pamoja
na uhuru wa mtu kujieleza. Hadi kufikia hatua hii, wananchi wa Zimbabwe wametoka jasho
kweli kweli!