Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa juma, alipata nafasi kwa mara nyingine tena
kutembelea Pango la Bikira Maria wa Lourdes, lililoko kwenye Bustani maarufu za Vatican
na kusali kwa kitambo, akiomba msaada wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa anapoanza
utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika hija hii ya kiroho, Baba Mtakatifu
alisindikizwa na viongozi waandamizi wa wa Vatican na baadaye alirejea kwenye makao
yake ya muda yaliyoko Domus Sanctae Marthae.
Itakumbukwa kwamba, Ijumaa, jioni,
Baba Mtakatifu Francisko alimtembelea Kardinali Jorge Maria Mejia, Mkutubu mkuu mstaafu
wa Maktaba ya Kanisa Katoliki, aliyelazwa kwenye Hospitali ya Pio wa kumi na moja.
Hii ilikuwa ni mara ya pili, kwa Baba Mtakatifu Francisko kutoka mjini Vatican kwa
ajili ya shughuli za kitume lakini katika hali ya faragha. Alipata nafasi ya kuweza
kuzungumza na Kardinali Mejia kwa muda wa dakika ishirini.
Baba Mtakatifu alipata
pia fursa ya kuwatembelea, kuwaona na hatimaye, kuwabariki wagonjwa waliokuwa wamelazwa
kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Wachunguzi wa mambo wanasema, yote haya yanaonesha
ile hali ya unyenyekevu, upendo na mshikamano wa kibaba kwa maskini, wagonjwa na wote
wanaoteseka kiroho na kimwili, anapania kuwaonjesha ile huruma na upendo wa kibaba,
kama ambavyo Kristo mwenyewe alivyofanya wakati wa maisha na utume wake hapa duniani.
Ni mfano na kielelezo cha kuigwa, kwani watu wengi katika ulimwengu mamboleo
wanataka ushuhuda wa maisha, kwani walimu wako wengi kiasi kwamba, hawana hata kazi!
Hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika
waamini na watu wenye mapenzi mema kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia
ya sala.