2013-03-20 08:43:38

Maskini hata katika umaskini wao wanaweza kuchangia kwa hali na mali kulistawisha Kanisa


Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, kwake binafsi anaona kwamba, kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu Francisko kuliongoza Kanisa Katoliki ni paji la Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Ulimwengu mamboleo na kwa namna ya pekee kwa Kanisa Barani Afrika. RealAudioMP3

Katika ulimwengu mamboleo watu wamefikia hatua ya kudhani kwamba, kwa nguvu ya fedha, mali na uchumi wanaweza kufanya jambo lolote hapa duniani. Baba Mtakatifu Francisko ni baraka kwa Kanisa, hali inayojionesha hata katika uchaguzi wa jina lenyewe. Ni Mtakatifu aliyezaliwa na kulelewa katika familia iliyobahatika kuwa na utajiri mkubwa.

Baada ya kuongoka akaacha yote na kujitosa pamoja na wenzake kumjengea Kristo Kanisa. Mwanzoni alidhani ni Kanisa la mawe, lakini pole pole alitambua kwamba, Kanisa alilokuwa anapewa changamoto ya kulijenga ni Fumbo la Mwili wa Kristo, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayojikita katika ufukara kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Pengo anakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu ana njia zake na kamwe hawezi kufungwa na fikara na mawazo ya binadamu. Uamuzi wa Francisko ulikuwa ni mzito, kiasi kwamba, baba yake mzazi aliamua kufukuza kutoka nyumbani kwake.

Francisko akapewa changamoto ya kulijenga Kanisa la Kristo lililokuwa limeanza kumezwa na malimwengu,kwa kutaka mambo ya ufahari na mali, katika ulimwengu wa wakati ule! Watu walipima mafanikio kwa wingi wa mali na madaraka aliyokuwa nayo mtu, wakasahau kwamba, madaraka ni kwa ajili ya kuwahudumia wanyonge na maskini na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chimbuko la mafanikio ya binadamu.

Kardinali Polycarp Pengo anasema, Baba Mtakatifu Francisko alikwisha kuona na kuonja hadha ya umaskini na mahangaiko ya watu wa Argentina. Akatambua kwamba, hawa ndio tegemeo la Kanisa. Akajitosa bila ya kujibakiza hata kidogo, akasimama kidete kulinda na kuwatetea maskini, ambayo kwa uhuru kamili amethubutu wawepo kwenye Ibada ya Misa Takatifu alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko hata baada ya kuchaguliwa kwake, maneno yake ya kwanza kwanza yanayonesha changamoto kwa Kanisa katika kuwahudumia maskini na kwamba, uongozi hauna budi kuwa ni huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni changamoto ambayo imeendelea kusikika hata katika Mahubiri yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Siku ya Jumanne, tarehe 19 Machi 2013.

Kardinali Polycarp Pengo anasema, Waamini Barani Afrika hata katika umaskini wao, wanaweza kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika. Hakuna sababu ya kukata tamaa na kwamba, umaskini au ufukara wa Kiinjili si jambo linaloweza kuwa ni kikwazo cha kuchangia maendeleo ya Kanisa Barani Afrika.

Hii ni changamoto kwa waamini Barani Afrika kushikamana na kujifunga kibwebwe kutumia karama na vipaji walivyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa na Jamii kwa ujumla wake. Wawe tayari kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu na kamwe kisiwepo kisingizio tena!

Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM anahitimisha mahojiano haya maalum na Radio Vatican kwa kutolea ushuhuda jinsi ambavyo hata Makardinali walivyopigwa na butwaa walipomwona Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kushirikiana nao kwa sala, chakula na maongezi kama ndugu bila ya kujitenga, changamoto kubwa kwa sasa ni kumsikiliza, kuona na kutenda kadiri ya maongozi yake!







All the contents on this site are copyrighted ©.