Papa Francisko ni nyota ya matumaini kwa wakimbizi na wahamiaji, wenye kiu na njaa
ya haki, amani, msamaha na upatanisho!
Mheshimiwa Padre Peter Balleis, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Wayesuit kwa ajili ya
kuwahumia wakimbizi anasema, wamepokea kwa mikono miwili habari za kuchaguliwa kwa
Baba Mtakatifu Francisko kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni kiongozi ambaye ameonja
hadha ya kuishi uhamishoni, kumbe atakuwa ni kielelezo cha matumaini kwa wakimbizi
na watu wasiokuwa na makazi maalum wanaonesha kiu na njaa ya haki, amani, upendo na
mshikamano wa dhati.
Hili ni kundi kubwa la watu wanaotaka kuonja upendo na
msamaha wa kweli, mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuyakazia katika
maisha na utume wake. Anatoa mwaliko kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linawashirikisha
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waweze kuona huruma na upendo wa Mungu
katika maisha yao.
Hawa ni wale ambao Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuhudumia
wakimbizi limekuwa likitenda kama sehemu ya utume wake. Ikumbukwe kwamba, waathirika
wakubwa ni wanawake na watoto, wanaopaswa kweli kupewa kipaumbele cha kwanza; kwa
kuheshimu na kuthamini utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuanza safari
ya udugu na upendo miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ndiyo changamoto ambayo
Baba Mtakatifu Francisko anapenda pia kuwashirikisha waamini wote kama njia ya kukuza
na kuimarisha haki inayojionesha katika imani tendaji.
Unyenyekevu, upole
na umakini kwa wote wanaoteseka ni kati ya fadhila ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia
Papa Francisko, ambaye ameguswa na mateso na mahangaiko ya wananchi wa Argentina.
Wayesuit
wanasema, kuna watu wengi wenye kiu na njaa ya haki, njaa ya ulinzi na usalama, wanaohitaji
kuonja upendo na msamaha wa kweli, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda na
kutetea: mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Ni matumaini ya wengi kwamba,
Baba Mtakatifu Francisko atasaidia kuwaonjesha watu waliokata tamaa katika maisha,
matumaini na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo, mchungaji mkuu.