Papa Francisko na Bartolomeo wa kwanza wakumbatiana; changamoto ya kusonga mbele katika
majadiliano ya kiekumene!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel
Gandolfo amefuatilia kwa njia ya Luninga, Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba
Mtakatifu Francisko, mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Itakumbukukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, yuko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, tangu alipoamua kwa utashi na
uhuru kamili kung'atuka kutoka madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013.
Kwa
mara ya kwanza katika historia ya Kanisa tangu ulipotokea Mpasuko wa Kanisa kunako
mwaka 1054, takribani miaka elfu moja iliyopita, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa
Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli amehudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu,
Khalifa wa Mtakatifu Petro anapoanza utume wake rasmi. Baba Mtakatifu Francisko na
Patriaki Bartolomeo wa kwanza, wamekutana kwa mara ya kwanza walipokuwa wanapeana
busu la amani, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Papa Francisko.
Patriaki
Bartolomeo amenukuliwa akisema kwamba, Makanisa haya mawili kadiri ya siku zinazovidi
kusonga mbele yanazidi kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayopania kujenga na kuimarisha
umoja wa Wakristo. Majadiliano kati ya Makanisa haya mawili yanajikita katika taalimungu
na dhamana na nafasi ya Papa katika maisha na utume wa Kanisa.