Papa Francisko anawachangamotisha waamini Kuinjilisha kwa njia ya matendo!
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu
anasema kwamba, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisco wakati huu
anapouanza rasmi utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kujitosa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya, kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Ni
mwaliko wa kuwaendea watu mahali walipo, ili waweze kuonja kwa mara nyingine tena
ile furaha ya Habari Njema ya Wokovu inayopata chimbuko lake kwa Kristo aliyeteswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Kardinali Filoni anasema, kwa sasa Mama
Kanisa anawachangamotisha waamini kujitosa kwa ari na bidii zaidi kumtangaza Kristo,
hasa kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; hawa
wanapaswa kuonjeshwa huruma na upendo wa Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko
anaendelea kuwahimiza Makleri na Familia ya Mungu kwa ujumla, kujiondoa kutoka katika
ubinafsi, raha na starehe na kuanza hija ya kuwatangazia watu upendo, furaha na matumaini,
kwa wote wale wanaoogelea katika dimbwi la umaskini wa kipato na maisha ya kiroho!
Kardinali
Filoni anawaalika waamini kuonesha mshikamano na upendo wa pekee kwa Baba Mtakatifu
Francisko kwa njia ya huduma kwa maskini. Baba Mtakatifu Francisco amekuja kwa wakati
wake, Mama Kanisa anapoendelea na hija ya kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya
dunia. Haya ni matunda ya sala na kazi ya Roho Mtakatifu, iliyowawezesha Makardinali
katika mkutano wa uchaguzi.
Huu ndio ushuhuda uliotolewa na Mama Theresa wa
Calcutta enzi ya uhai wake, ushuhuda wa Injili unaotekelezwa na waamini sehemu mbali
mbali za dunia. Jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi linaonesha fadhila ya unyenyekevu,
ari na moyo wa Uinjilishaji.