Papa Francisko amtuma Kardinali Pengo kuwaimarisha ndugu zake katika imani Visiwani
Zanzibar
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Madagascar ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, hivi karibuni alipokutana na Baba Mtakatifu
Francisko, alimtuma kwenda Zanzibar ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani.
Kutokana
na agizo hili, Kardinali Polycarp Pengo, anatarajiwa katika maadhimisho ya Jumapili
ya Matawi, kushiriki na waamini wa Jimbo Katoliki Zanzibar kwa Ibada inayoliingiza
Kanisa katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Kardinali
Polycarp Pengo anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwombea Baba Mtakatifu
Francisko, ili Mwenyezi Mungu aweze kumlinda na kumwiimarisha katika utekelezaji wa
malengo yake ya kitume. Papa Francisko akiishaimarika katika imani, matumaini na mapendo,
aweze pia kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo, hasa wale wanaoishi katika wasi wasi
na hofu ya madhulumu ya kidini. Wasikie na kuonja uwepo na sala za Baba Mtakatifu
Francisko katika hija ya maisha yao hapa duniani, kamwe wasidhani kwamba, wamesahaulika!