2013-03-19 08:12:50

Baba Mtakatifu Francisko ni tumaini la maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii!


Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hispania, Manos Unidas ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kuonesha ushuhuda wa imani katika matendo kwa kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali zao za maisha, linasema kwamba, lina matumaini makubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, kwani ameonesha tangu awali wa mapambazuko ya utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wahitaji zaidi.

Manos Unidas linachukua fursa hii kutoa mwaliko kwa Mashirika pamoja na Jumuiya ya Kimataifa, kuendelea kulivalia njuga tatizo la umaskini, magonjwa na ujinga, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kila mtu akitekeleza dhamana na majukumu yake, inawezekana kabisa Jumuiya ya Kimataifa kupunguza hali ya umaskini wa hali na kipato mintarafu Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ifikapo mwaka 2015.

Changamoto hii ambayo kwa wengi inaonekana kuwa ndoto inawezeka kufikiwa, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni miongoni mwa watu, daima wakitafuta mafao ya wengi, haki, amani, udugu na mshikamano wa kimataifa. Hizi ni kati ya fadhila ambazo zinapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko anapoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.