Rais Robert Mugabe, kuhudhuria sherehe ya Papa Francis anapoanza utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro
Wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameanza kuwasili mjini Vatican kwa ajili
ya kushuhudia Baba Mtakatifu Francis akianza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu.
Katika hotuba zake ambazo zinaonesha dira na mwelekeo wa maisha na utume wake, anaendelea
kukazia umuhimu wa waamini kutembea katika mwanga wa Kristo, wakijenga na kuliimarisha
Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Anasema kwamba, Kanisa halina budi kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya maskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira.
Kati
ya viongozi mashuhuri kutoka Barani Afrika ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye
kwa kawaida matukio kama haya yanayogusa masuala ya imani hakosekani kamwe. Itakumbukwa
kwamba, kunako mwaka 2011 wakati Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alipokuwa
anamtangaza Yohane Paulo wa Pili kuwa Mwenyeheri alifika bila wasi wasi wowote, akisema
kwamba, alikuwa na ibada ya pekee kabisa kwa Papa Yohane Paulo wa Pili.
Wakati
wa maziko ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, kunako mwaka 2005 alitinga mjini
Vatican licha ya kuwekewa vikwazo na Jumuiya ya Ulaya. Kunako mwaka 2008 Rais Mugabe
alihudhuria pia mkutano wa FAO uliokuwa unafanyika mjini Roma.
Baadhi ya viongozi
wakuu wa Serikali waliokwishawasili ni pamoja na Rais Cristina Fernandez Kirchner
wa Argentina na Rais Sebastian Pinera kutoka Chile. Watu wengine mashuhuri ni Bwana
Perez Esquivel mshindi wa tuzo ya amani kutoka Argentina anasisitiza kwamba, Kardinali
Bergoglio enzi ya utumishi wake nchini Argentina, hakuwahi kuunga mkono utawala wa
mabavu nchini humo.
Marais wengine waliowasili tayari ni Taur Matan Ruan kutoka
Timor ya Mashariki.