2013-03-18 16:12:14

Papa Francis asema, Kristu hachoki kusamehe maovu yetu...


Jumapili katika kuiadhimisha Jumapili ya Tano ya kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu Francis, aliongoza Ibada ya Misa, katika Kanisa la Mtakatifu Anna, Mama wa Bikira Maria liliko ndani jijini Vatican. Hii ilikuwa ni Ibada yake ya kwanza, kuadhimisha mbele ya waaumini wa kawaida, tangu kuchaguliwa kuwa Papa. Katika Ibada hiyo alitoa mwaliko kwa watu wote kuikimbilia huruma ya Mungu bila woga wala kuchoka.
Ibada hii, inayotajwa ya kupendeza, pia inasemekana kwamba ilikuwa na mvuto wa kipekee kwa wanaparokia. Papa Francis, katika homilia yake, aliwaonya waamini dhidi ya tabia za kusijifu na kujiona kuwa na maana na haki mbele ya Bwana kuliko wengine na hasa wadhambi, wasioamini , na wenye kiu ya kutaka kumjua Mungu. Alionya kwamba, hatujui Bwana anachofikiri juu watu hao.
Homilia ililenga katika somo la Injili , ambamo Yesu aliingilia kati, wakati mafarisayo na wanasheria walipotaka kumpiga mawe mwanamke hadi kifo. Aliwaaambia yeyote asiyekuwa na dhambi na awe wa kwanza kumrushia mwanamke huyu jiwe. Hakuna aliyejitokeza badala yake wote waliondoka kimya kimya. Na Yesu alimwonea huruma mwanamke na kumwambia, nenda zako, usitende tena dhambi.
Alisema, pengine si jambo jepesi mtu kutambua wingi wa huruma hii ya Mungu , ambayo haina kipimo. Lakini Bwana iliyejaa huruma, humkumbatia kila mmoja na wala hahukumu, ila hutuonya tu pale tunapotenda dhambi. HIvyo binadamu anapaswa kuikimbilia neema ya Mungu bila kuchoka, kwa kuwa Bwana hachoki kusamehe.
Mwishoni mwa Ibada, licha ya ulinzi mkali, Papa aliwakaribia waamini na kusalimiana nao,akiwemo Paroko wa Parokia hiyo, Padre Bruno Silvestrini OSA, na pia Padre Mkuu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na Vika Mkuu wa Jiji la Vatican, Kardinali Angelo Comastri. Aliishukuru jumuiya zima ya Parokia hiyo na wale wote waliofunga safari hadi Roma katika siku hizi, akimtaja Padre Gozalo Aemilius , Mkurugenzi wa Taasisi ya Jubilar Pablo 11 toka Uruguay, inayo shughulika na utoaji wa elimu kwa watu masikini na hasa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, Uruguay.
Na maelfu walijumuika kusali Sala ya Malaika wa Bwana na Papa ..
Wakati wa adhuhuri, kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake, Baba Mtakatifu Francis aliongoza Sala ya Malaika wa Bwana, tokea dirisha la Jengo la Kipapa, kama ambavyo imekuwa utaratibu wa Mapapa wote, kusali na kusalimia waamini mahujaji na wageni wanaofika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili mchana, kwa ajili ya sala ya Malaika wa Bwana. .
Papa Francis , katika hotuba yake fupi kwa umati wa watu wanaokadiriwa kufikia 300.000, waliokuwa wamekusanyika, licha ya hali mbaya ya hewa, mvua na baridi, aliuasa umati huo, kwamba, kamwe Neema ya Mungu haimkatii tamaa mdhambi. Bwana kamwe , hachoki kusamehe, ni sisi ambao tunachoka kuomba msamaha.
Wakati huo pia , Papa alirejea soma la Injili ya Jumapili, (Yn 8:1-11), juu ya mwanamke mzinzi,akisema, Yesu hakumtolea mwanamke maneno ya dharau au kumhukumu, lakini aliongea na mwanamke kwa maneno ya upendo na huruma, yaliyo mwalika katika uongofu wake: "'Wala mimi sikuhukumu, Nenda, na kuanzia sasa usitende dhambi tena ".
Pia Papa , alikitaja kitabu cha Mwanateolojia Kardinali Walter Kasper , Mstaafu Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Kukuza Umoja Wakristu, aliyemwita kuwa “Mwanateolojia Mkuu", huku akisema, si kama anatangaza kitabu cha Kardinali Kasper , lakini kwamba, kazi iliyochapishwa katika kitabu hicho 2012 chini ya jina la Kijerumani "Barmherzigkeit" (Rehema),imekuwa msaada mkubwa kwake.
Alieelza , katika Kitabu hicho Kardinali Kasper ameandika kwamba , kuisikia huruma ya Mungu , ni hisia zinazobadilisha hali zote za ndani ya maisha ya kiroho. Na huruma kidogo, huleta dunaini fukuto na haki zaidi.
Papa Francis alieleza na kuyakumbuka maneno aliyo ambiwa miaka 20 iliyopita na mwanamke mmoja mzee wa Buenos Aires, kwamba, "kama Bwana hasamehi yote, dunia isingekuwepo".
Maneno hayo ya hekima ya mama huyo mkongwe yalimgusu Papa Francis, na kutaka kumwuliza iwapo Bibi huyo ni mhitimu wa Chuo Kikuu maarufu cha Kipapa ya Gregorian cha mjini Roma, kwa sababu maneno yake, yalikuwa yamejaa hekima inayotoka kwa Roho Mtakatifu, juu ya huruma ya Mungu"
Na baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa alisalimia katika lugha mbalimbali , kwa mara ingine, alieleza kwa kifupi kwa nini alichagua jina la Francis, kwamba, lina mpa nguvu za kiroho, na pia linajenga uhusiano na eneo la Mtakatifu Francis wa Assis, katika asili ya uzawa.
Baba Mtakatifu pia Jumapili akipeleka Ujumbe wake wa kwanza rasmi katika Ukurasa wa Tweet@pointifex, ametoa shukurani zake za dhati kwa wote akisema, “ Wapendwa Marafiki zangu, ninawashukuru nyote kwa moyo wa dhati, na naombeni mwendelee kuniombea”.







All the contents on this site are copyrighted ©.