Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox katika maadhimisho ya Kipindi
cha Kwaresima kwa Kanisa la Kiorthodox anawaalika waamini kuonesha upendo na mshikamano
na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao
ya maisha. Mshikamano huu ni muhimu sana kwa mwaka huu wa 2013, ambao kutokana na
athari za myumbo wa uchumi kimataifa, umetangazwa kuwa ni Mwaka wa Mshikamano wa Kimataifa.
Ni mwaliko wa kushirikishana na kugawana kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu amewakarimia
waja wake.
Katika ujumbe wake kwa Jumapili ya Msamaha, ambayo imeadhimishwa
na Kanisa la Kiorthodox, Jumapili, tarehe 17 Machi 2013, anawaalika waamini kwa namna
ya pekee kuonesha upendo kwa jirani zao, ili kujitajirisha katika maisha ya kiroho.
Ni mwaliko na changamoto ya kutosheka na kipato chao, waaminifu na waadilifu wa mali
ya umma. Kwa maneno machache anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza, waamini wanapaswa
kutolea ushuhuda wa maisha adili.
Lakini kwa bahati mbaya, ulimwengu mamboleo
unaonesha sura tofauti kabisa kwa watu kupenda mno mali, utukufu na madaraka. Katika
mahubiri yake, Mtakatifu Yohane Chrisostom anasema, hakuna jambo baya kuliko yote
ikiwa kwa mtu kutojua kupenda. Kwa mwelekeo huu wa maisha, hakuna mtu anayeweza kuguswa
na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zake. Waamini wajifunze kutekeleza matendo
ya huruma katika maisha yao, kwa kuwaonesha jirani zao upendo, huruma na faraja.
Patriaki
Bartolomeo wa kwanza katika mahubiri yake anabainisha kwamba, hakuna furaha kubwa
kama ile ya mtu kumwonjesha upendo jirani yake. Kwa bahati mbaya, mwalimu dunia anapenda
kuwafundisha vijana kupenda raha na anasa hata kupita kiasi, hali ambayo inapelekea
kinzani na migawanyiko katika Jamii. Jamii ijifunze kuonesha moyo wa upendo na mshikamano
wa kweli, kwa kusaidiana kwa hali na mali.
Kwaresima kiwe ni kipindi cha kusafisha
roho na mwili kwa kujikita zaidi katika upendo kwa Mungu na jirani; upendo ambao Yesu
mwenyewe amewaonesha wafuasi wake. Upendo huu hauna budi kuwa ni sehemu ya sadaka
na majitoleo ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Upendo ujioneshe katika matendo,
hasa kwa wakati huu, watu wengi wanapoendelea kuonja athari za mtikisiko wa uchumi
kimataifa.